Sikilizeni kilio cha watu wanaokufa kwa baa la njaa na lishe duni, ili kuokoa maisha
yao!
Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujenga umoja na mshikamano, ili kuibua mbinu mkakati
utakaosaidia kupambana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha sanjari na mabadiliko
ya tabianchi na kwamba, Kanisa kwa upande wake, linapania kumletea mwanadamu ustawi
na maendeleo endelevu, yanayogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili, lakini kwa
kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii,
ili usalama na utu wao viweze kulindwa.
Watu wanapaswa kutegemeana kama familia,
lakini ukweli wa mambo ni kwamba, kinzani za kiuchumi zimekuwa ni kitovu cha misigano
inayohatarisha urafiki wa kidugu, hali inayopelekea baadhi ya watu kutothaminiwa na
hatimaye, kutengwa; mambo yanayowatendea watu wasiokuwa na fursa za ajira au wale
wanaoteseka kutokana na baa la njaa. Hapa kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana,
ili kupambana na baa la njaa na lishe duni, kwa kutambua haki ya mtu kupata lishe
bora.
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi,
tarehe 20 Novemba 2014 kwa wajumbe wa Jumuiya ya Kimataifa wanaoshiriki katika mkutano
mkuu wa pili wa kimataifa unaojadili mikakati ya kupambana na baa la njaa pamoja na
lishe duni, ulioandaliwa na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO
kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani, WHO. Watu wengi leo hii wanazungumzia
kuhusu haki, lakini haki ya mtu kupata chakula inahodhiwa na nguvu ya soko na faida
kubwa, wakati mamillioni ya watu wanaendelea kufariki dunia kutokana na baa la njaa;
hili ni kundi ambalo utu wake unahitaji kuheshimiwa.
Baba Mtakatifu anasema
mbinu mkakati unaoibuliwa na Jumuiya ya Kimataifa wakati mwingine unaweza kubaki kama
nadharia, lakini watu wanahitaji kuona haki ikitendeka, kwa kutambua mahitaji msingi
ya binadamu; kwa kuheshimu na kuthamini haki za wale wanaoteseka kwa baa la njaa na
lishe duni, kwa kutekeleza haya, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kupata mafanikio makubwa
katika utoaji wa misaada na utekelezaji wa mikakati ya maendeleo endelevu.
Uzalishaji,
upatikanaji wa chakula, mabadiliko ya tabianchi na soko la mazao ya kilimo ni mambo
yanayopaswa kuongozwa na kanuni za kitaaluma, lakini, binadamu na mahitaji yake msingi
anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Kuna chakula kingi kinachozalishwa ambacho
kinaweza kutosheleza mahitaji ya watu duniani kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane
Paulo II, lakini bado kuna kiasi kikubwa cha chakula kinaharibika na kutupwa wakati
kuna mamillioni ya watu wanakufa kwa baa la njaa na lishe duni.
Baba Mtakatifu
anasema, haya ni matokeo ya kuchakachuliwa kwa taarifa na takwimu muhimu; usalama
wa taifa, rushwa na ufisadi na mbaya zaidi, ni madhara ya myumbo wa uchumi kimataifa.
Hii ni changamoto ya kwanza ambayo Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuipatia ufumbuzi
wa kudumu katika mapambano ya baa la njaa duniani.
Ukosefu wa mshikamano ni
changamoto ya pili inayopaswa kufanyiwa kazi kwa kufisha ubinafsi na migawanyiko,
mambo yanayowaathiri wanyonge kiasi hata cha watu hawa kuchukia Serikali zao. Mshikamano
ni mchakato unaowawezesha watu kukutana na kusaidiana kwa hali na mali; kwa kujenga
mahusiano bora, wote wakidhamiria kutafuta mafao ya wengi.
Binadamu wanapaswa
kutambua kwamba, wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kuwa wanawajibika fika
kulinda na kutunza mazingira, changamoto ya kushikamana kwa dhati badala ya kupigana;
mambo yanayoitumbukiza dunia katika umaskini. Mwenyezi Mungu anaweza kumsamehe binadamu
kutokana na dhambi zake, lakini, dunia kamwe haiwezi kumsamehe mwanadamu, atalipa
hadi senti ya mwisho!
Serikali zitambue kwamba, ni mkusanyiko wa Jumuiya ya
Watu, zinazopaswa kusaidiana, kwa kuzingatia sheria na kanuni za kimataifa, huku zikiongozwa
na sheria asilia ambayo inaweza kueleweka na wengi kwani inazungumza lugha ya: upendo,
haki, amani, mambo msingi yanayokumbatiana. Kama ilivyo kwa binadamu, Serikali na
Mashirika ya kimataifa hayana budi kujenga moyo wa majadiliano na utamaduni wa kusikilizana
na kwa njia hii, lengo la kufuta baa la njaa na utapiamlo duniani linaweza kufikiwa!
Serikali
hazina budi kutekeleza wajibu wake kwa kutafuta na kulinda mafao ya raia wake bila
ya kujibakiza hata kidogo, jambo linalohitaji utekelezaji na udumifu. Kanisa Katoliki
linaendelea kuchangia katika ustawi na maendeleo ya watu kwa kutoa kipaumbele cha
kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa kushirikiana na
Jumuiya na Mashirika ya Kimataifa, ili kusaidia mchakato wa mikakati ya maendeleo
inayozingatia usawa na kanuni msingi kama vile: ukweli, uhuru, haki na mshikamano
pamoja na kutambua haki ya chakula, uhai na maisha bora zaidi; ni haki ya kulindwa
kwa mujibu wa sheria na kwamba, ni sheria maadili ili kuweza kushirikishana utajiri
wa uchumi wa dunia.
Baba Mtakatifu anasema kwa wale wanaoamini kwamba, umoja
wa Familia ya binadamu unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Muumbaji na
udugu miongoni mwa binadamu; hakuna maelezo yoyote yale ya kiuchumi na kisiasa yanayoweza
kukubalika kwa kuona watu wanakufa kwa baa la njaa na lishe duni.
Mfumo wa
kibaguzi kwa hali na haki hauna budi kuwekwa pembeni katika soko la chakula duniani
na kamwe usiwe ni mfano wa mikakati katika kupambana na baa la njaa duniani. Baba
Mtakatifu anawasihi viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza kilio cha watu wanaokufa
kwa baa la njaa na lishe duni, ili kutoa chakula kitakachosaidia kuokoa maisha ya
watu wengi duniani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.