2014-11-20 07:37:06

Pambaneni na umaskini na kulinda mazingira!


Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kujipanga vyema ili kuweka bayana mikakati ya maendeleo endelevu itakayofanyiwa kazi mara baada ya kukamilika kwa Malengo ya Mendeleo ya Millenia hapo mwaka 2015, kwa kujikita zaidi katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini wa kutupwa; kwa kulinda na kutunza mazingira.

Hizi ni changamoto kubwa ambazo Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kupambana nazo, ili kudhibiti madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaendelea kutishia usalama wa maisha ya watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuanza kutekeleza malengo yake ili kudhibiti hewa ya ukaa inayozalishwa kwa wingi kutokana na teknolojia isiyokuwa rafiki kwa mazingira.

Akichangia hoja kwenye mkutano mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa uliokuwa unajadili kuhusu mikakati ya maendeleo endelevu na utunzaji bora wa mazingira, Askofu mkuu Benedito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema kwamba, utunzaji bora wa mazingira ni sehemu muhimu sana ya uwajibikaji wa kimaadili na haki. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujiandaa kikamilifu katika mkutano wa tabianchi unaotarajiwa kufanyika mjini Paris, Ufaransa, Desemba 2015.

Jumuiya ya Kimataifa itambue kwamba, watu wote wanategemeana, hata matajiri wanawategemea maskini na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kupata mafanikio makubwa, ikiwa kama watashikamana kwa pamoja kutekeleza Itifaki ya mwaka 2020 inayopania kupunguza hewa ya ukaa kwa kiasi kikubwa, kwa kutambua kwamba, watu wanawajibika kutunza mazingira kama sehemu ya haki msingi za binadamu. Utunzaji wa mazingira uwe ni kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya watu wachache katika jamii, changamoto ya kubadili mtindo wa maisha kwa kuwajibika zaidi.

Askofu mkuu Auza anasema, dunia kwa sasa inaonekana kuwa kama kijiji, kumbe, kuna haja ya kuwa na uwajibikaji wa pamoja, dhamana inayopaswa kutekelezwa na Serikali pamoja na watunga sera, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora kwa sasa na kesho yenye matumaini makubwa zaidi. Utunzaji bora wa mazingira unahitaji sera na mikakati makini ya kiuchumi inayopangwa na kutekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa, kwa kuzingatia kanuni msingi za kimaadili na kisayansi.








All the contents on this site are copyrighted ©.