2014-11-20 11:54:29

Jipambanueni si tu katika weledi, bali katika utu, upendo na huruma kwa maskini!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuhutubia mkutano mkuu wa pili wa kuhusu lishe, Alhamisi, tarehe 20 Novemba 2014, alipata nafasi ya kukutana pia na kusalimiana na wafanyakazi wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO na kuwataka kudumisha upendo na maelewano na wale wote wanaoishi nao ndani ya familia na sehemu zao za kazi.

Baba Mtakatifu amewapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Makao Makuu ya FAO kwani kutokana na matukio mbali mbali yanayofanyika FAO, wanapata bahati ya kukutana na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaofika ili kupanga sera na mikakati ya kupambana na baa la njaa na lishe duni duniani. Wafanyakazi hawa wana bahati ya kugusa matatizo na mahangaiko ya watu wenye haki ya kupata maboresho ya maisha.

Baba Mtakatifu anawashukuru kwa huduma makini wanayoitoa katika ukweli wa kimataifa, unaolenga kupambana na baa la njaa, ili kukuza na kudumisha sekta ya kilimo na uzalishaji wa chakula. Anatambua mshikamano wao na watu wenye njaa, lishe dunia na kiu, changamoto ya kupeta si tu katika weledi, bali katika utu, upendo na huruma kwa kuonesha mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kufuata mfano wa Yesu, aliyejinyenyeza hata kujitwalia hali ya ubinadamu, kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu.

Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi wa FAO kutokata tamaa wanapokumbana na magumu, bali wasaidiane, ili waweze kwa pamoja na kumwelekeo wa kesho yenye matumaini. Baba Mtakatifu amewahakikishia sala zake na kuwamba wao pia kumkumbuka katika sala anapotekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.







All the contents on this site are copyrighted ©.