2014-11-20 08:46:17

Jimbo Katoliki Musoma, kufunga Sinodi ya Jimbo, tarehe 23 Novemba 2014


Sinodi Musoma, Imani na matendo, ndiyo kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania, kama fursa ya kuifahamu, kuikiri, kuiadhimisha, kuuishi na kuitangaza kwa matendo. Sinodi hii ilizinduliwa rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, hapo tarehe 19 Mei 2013 na inafungwa rasmi, tarehe 23 Novemba 2014, Mama Kanisa anapoadhimisha Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. RealAudioMP3

Maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Jimbo Katoliki la Musoma ni matokeo ya Jubilee ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, muda muafaka wa kutathmini ukomavu wa Jimbo na kupanga mikakati ya kuliwezesha Jimbo kusonga mbele kwa imani na matumaini. Jimbo Katoliki Musoma, hivi karibuni liliadhimisha Jubilee ya Miaka 100 ya Ukristo, muda muafaka wa kupima jinsi ambavyo Kanisa mahalia limepokea na kuendelea kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Sinodi ya kwanza na ya Pili kwa Bara la Afrika ilikuwa na changamoto nyingi ambazo zinapaswa kuendelea kufanyiwa kazi na Makanisa mahalia, ili kweli Kanisa Barani Afrika liwe ni chombo cha upatanisho, haki na amani. Jimbo la Musoma limepembua na kuangalia ni kwa jinsi gani mafundisho yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi za Afrika yamemwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo Katoliki Musoma. Sinodi hii imeadhimishwa wakati Kanisa lilikuwa linaadhimisha pia Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kuchapishwa kwa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki pamoja na kuchapishwa kwa Gombo la Sheria za Kanisa, matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Askofu Michael Msonganzila, alikuwa pia na nafasi ya pekee katika maadhimisho haya kwani anafanya kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipoteuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kuliongoza Jimbo Katoliki Musoma na kusimikwa hapo tarehe 20 Januari 2008.







All the contents on this site are copyrighted ©.