2014-11-20 15:29:20

Chezea mengine, laana ni kiboko chao!


“Laana” inatisha sana. Nimewahi kumsikia mama mmoja akimfokea binti yake baada ya kutukanwa naye matusi machafu akimwambia: “Nitakulaani”. Usemi huu unaonekana kuwa na ukweli pale unapomwona binti aliyelaaniwa akitembea na gauni la Eva pindi nguo nyingine zote amezifunga kichwani.

Ukiwauliza watu kulikoni? Wanakujibu kifupi tu: “ni laana ya wazazi hiyo”. Kadhalika yaweza kumtokea mtu aliyekuwa na heshima zake na kazi nzuri, baada ya kuingia katika ulimwengu wa raha, wa kulewa sana, na kuvuta bangi, kisha anapoteza utu wake na kuruka kichaa. Watu wanaweza kusema: “Kalaaniwa na Mungu” au “Kalogwa”.

Fikra namna hii ya “kulaani” ipo katika maisha yetu na katika akili zetu hasa kwa utamaduni wa mwafrika. Kadiri ya mila na desturi zetu, yeyote anayeenda kinyume na matakwa ya wazazi wake huyo hupata laana. Kadhalika anayemkufuru Mungu anaweza kupata laana. Fikra hizo za laana haziko tu kwa Waafrika peke yao, unaweza kuona pia katika utamaduni wa mataifa mengine hapa duniani.

Leo tunahitimisha mwaka wa Liturujia kwa kuadhimisha sikukuu ya Kristu Mfalme. Tunapambana na usemi huu wa “kulaani” ukitamkwa na Yesu mwenyewe: “Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake”. Semi aina hii zinazotisha zimenukuliwa karibu mara sita katika Injili ya Matayo.

Picha aina hii juu ya hukumu ya Mungu inahubiriwa pia na baadhi ya wachungaji, hasa wanapotaka kuwatisha watu juu ya yatakayowatokea itakapowabidi kutoa hesabu za maisha mbele ya kiti cha hukumu ya Mungu. Matokeo yake kule kukutana na Mungu ambako kila mtu anakungojea kwa hamu, kunaletesha woga sana, hasa kwa mtu mwovu na mtenda dhambi. Kadhalika kwa raia wa kawaida, mambo yanapowaenda ovyo, yaani kunapotokea mauaji, kukosewa haki, ujambazi, magonjwa, kuonewa, njaa na kiu, hapo utasikia watu wanasema: “Hii ni laana toka kwa Mungu” au “viongozi wetu ni laana mtupu”.

Ukweli ni kwamba, Mungu anayehukumu hivyo, anatushangaza na kututisha sote hasa sisi wakristu. Namna hii ya kumtazama Mungu ni potovu kabisa. Injili maana yake ni Habari njema, kwa hiyo ni bahati mbaya sehemu hii inatafsiriwa vibaya tena kwa haraka na kwa juu juu. Tafsiri namna hiyo inatupatia picha ya Mungu na ya Yesu Kristu inayojipinga yenyewe.

Jaribu kuona jinsi hali zinavyokinzana na kupingana zenyewe juu ya Mungu na Kristu wake: Kwa mfano, unawezaje kuunganisha pamoja hali ya huyu Mwana wa Mungu aliye mwema kwa wote, na sasa anabadili hali yake ya wema na kuchukua tabia ya hakimu mkali anayetisha, au yawezekanaje Mungu anayeangazisha jua wema na wabaya, anayenyeshesha mvua watu wote bila ubaguzi sasa abadilike na kuwa hakimu mbaya kwa watoto wake.

Yesu aliyesema, muwe kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mwema, asiyetenganisha wala kupendelea mtu yeyote, huyu Mungu aliyewakomboa watu wote, anawezaje sasa kufanya ubaguzi kama huu wa kutenganisha watu wema na wabaya. Unadhani Mungu huyu ataweza kweli kufurahi, atakapoona baadhi ya watoto wake wanateseka motoni kwa sababu ya uchaguzi wao wa ovyo. Ukweli ni kwamba Mungu ni mwenye haki na mapendo yanayodumu milele. Kutokana na mashaka na maswali namna hiyo tunaweza kuanza kuelewa kidogo maana ya Injili ya leo.

Ujumbe wa Yesu tunaanza kuuona katika maingilio yasemayo: “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake”. Huyu Mwana wa Adamu ndiye anayehukumu. Anakuja kupima endapo maisha ya ubinadamu huu yamefanikiwa kulingana na maisha ya Mwana wa Adamu. Yesu ndiye atakayekuwa kipimo cha maisha yetu na siyo kulinganisha ufaulu wa binadamu na vigezo vya ufaulu wa kiulimwengu huu.

Kwa hiyo kituko cha hukumu kilichooneshwa katika Injili ya leo siyo mfano, bali ni onesho la chumba cha mahakama. Onesho aina hii unaweza kuliona pia katika kitabu cha Daniele sura ya saba pale wanavyojitokea watawala wa ulimwengu huu kwa mfano wa wanyama wakubwa wanne toka baharini: “simba mwenye mabawa ya tai, dubu, chui, ndege”, halafu linafuata onesho la hukumu ilipoandikwa, “Hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa.” Onesho aina hili la hukumu unaiona pia kwa watu wa mashariki katika Kitabu cha wafu wanapopima roho ya mtu siku ya hukumu.

Katika onesho la mahakama toka Injili ya leo, kuna pande mbili zinazohojiwa. Kuna watu wa mkono wa kulia na wale wa mkono wa kushoto. Pande zote zinafuata mfumo unaolingana wa mahojiano. Kwanza inatolewa hukumu, halafu zinatolewa hoja za hukumu, kisha hufuata majiteteo au upinzani, halafu kunatolewa tamko la mwisho.

Hakimu ambaye ni Mfalme, ni Mwana wa Adamu, ndiye anayetathmini nani kati ya binadamu yuko upande wa ufalme mpya wa binadamu. Anaanza kutoa hukumu kwa wale wa upande wa kulia: “Njoni mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu”. Baada ya hukumu anatoa hoja kwa nini wanapata hukumu ya baraka hiyo: “Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula, nalikuwa na kiu, mlininywesha, nalikuwa mgeni mkanikaribisha, nalikuwa uchi mkanivika, nalikuwa mgonjwa mkaja kunitazama, nalikuwa kifungoni mkanijia.” Baraka maana yake ni maisha mema ya utu. Halafu itafuata "longolongo nyingi" ambayo ni mshangao. Hao wenye haki wanashangaa walichokifanya. Wanauliza ni wapi walipomfanyia mfalme haya yote? Yesu anajibu, “kwani mlipofanya hivi kwa mmoja wa wadogo mmenifanyia mimi.”

Sasa fuatilieni vizuri hukumu inayotolewa anapowageukia wale wa mkono wa kushoto anasema: “Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;” Hapa haisemwi kama ilivyotamkwa kwa wale wema “Njoni mliobarikiwa na Baba yangu” Hapa napo tungetegemea ingesemwa pia kwa hawa waovu: “Ondokeni kwangu mliolaaniwa na Baba yangu”. La hasha, neno hili “Baba yangu” limeondolewa limebaki neno moja tu la “laana”. Maana yake Mungu haingii katika laana.

Neno hili “laana” hata kiafrika lamaanisha kuwa mtu wa nuksi, mtu wa mkosi, mtu aliyeharibikiwa, mtu asiye na maisha mazuri, mtu aliyejichanganya mwenye hasa baada ya kudhulumu wengine, kama vile jambazi, mwizi, mbugiaji unga, sasa maisha yanamwendea vibaya, amebaki kuzubaazubaa tu au kuchanganyikiwa na hana mwelekeo, kila amwonaye anasema: “mtu huyu amelaanika” maana yake mtu huyo amekosa mwelekeo. Amekosa utu hivi ameharibikiwa.

Hoja ya kupata laana hiyo ni matendo sita mema ya upendo yaliyotajwa ambayo hawakuyafanya: “kumlisha chakula mwenye njaa, kumnywesha mwenye kiu, kumkaribisha mgeni, kumvika aliye uchi, kumtazama mgonjwa, kumtembelea mfungwa kifungoni.” Kisha kunafuata majiteteo, au kupinga hoja na hawa wanaohukumiwa.

Mara nyingi zinaporudiwa tena hoja hizo mara mbili mbili, yaonekana kama inachosha kusikiliza, lakini kumbe ndiyo hapo palipojaa uhondo. Matendo haya sita ambayo Yesu anayarudiarudia ndiyo ujumbe anaotaka kuutoa, ujumbe ulio wa msingi na siyo suala la hukumu ya Mungu kama unavyoliona hapo. Yesu anataka kusisitiza kwamba matendo ya binadamu yatahukumiwa kutegemeana na vigezo hivi vya upendo. Hivi mara nne anarudia matendo haya ya upendo katika hali ya chanya na hasi.

Kuna mifano mingine mingi tu ya aina hiyo katika Injili, mathalani, mfano wa nyumba iliyojengwa juu ya mchanga na nyumba iliyojengwa juu ya mwamba. Kadhalika Heri maskini, halafu ole wenu matajiri. Barabara iliyonyoka na barabara isiyonyoka. Mwenye vazi la arusi na asiyekuwa na vazi la arusi.

Aaminiye na kubatizwa ataokoka asiyeamini atahukumiwa, nk. Hali hasi katika mifano hiyo haina maana nyingine zaidi ya kutoa msisitizo, yaani kusisitiza upendo. Maana yake maisha safi ya ubinadamu anayo yule anayependa, vinginevyo anajitafutia laana mwenyewe. Usambamba unaopingana unawekwa ili kusisitiza jambo.

Yesu anaposema: “Ondokeni kwangu”, ni tamko au hali anayoonesha mtu mwenyewe anapomtenga na kuacha kumtendea wema mhitaji, ni kama vile anamtenga na kumwambia: “hebu nitue, kaa mbali nami, tusijuane.” Lugha hiyohiyo ataitumia Kristo kwako kwani ulishamtenga alipojitokeza kwa wahitaji.

Kwa hiyo lengo la fasuli hii siyo hukumu, bali inataka kututafakarisha jinsi gani tunatakiwa kuishi maisha yetu leo. Kupitia vigezo hivi sita ambavyo ni vya kawaida hasa huko mashariki. Jambo jipya analoliingiza Yesu katika msisitizo huo, ni utu wake unaolinganishwa na mtu yule anayebarikiwa, yaani chochote chema kifanyikacho kwa mdogo hicho huunda upendo unaounganishwa na Kristu mwenyewe.

Mbele ya Mungu, kitu kimoja tu kitakuwa na maana nacho ni upendo. Aidha, kuhusu mbuzi (mbaya) na kondoo (mwema), ni kila mmoja wetu ni mbuzi pale tusipolingana na Kristo na ni kondoo kwa yule mwenye matendo yanayolingana na Mungu. Tujitahidi daima kuwa kondoo na kuishi maisha ya Kristo katika maisha yetu ya kila siku, vinginevyo ni unajilaani wenyewe.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.