Caritas Afrika katika kupambana na majanga asilia!
Shirika la Misaada Barani Afrika, Caritas Africa, hivi karibuni lilifanya mkutano
wake mkuu mjini Kampala, Uganda ili kuangalia pamoja na mambo mengine, taarifa ya
kikosi kazi katika kupambana na majanga mbali mbali Barani Afrika. Wajumbe walipata
nafasi ya kusikiliza taarifa ya shughuli za "Caritas Africa" kutoka katika nchi mbali
mbali pamoja na kuangalia mwongozo wa utendaji wa shughuli zake.
Wajumbe walipitia
mapendekezo ya mwongozo wa shughuli za "Caritas Africa" na kwamba, wajumbe watapewa
mwongozo rasmi baada ya marekebisho yaliyofanywa mwishoni mwa mwezi Agosti, 2014.
Caritas Africa imeangalia pia majanga mbali mbali yanayoendelea kujitokeza ndani na
nje ya Bara la Afrika na kwamba, Bara la Afrika halina budi kuweka kanuni maadili,
viwango vya uwajibikaji, ubora wa vifaa vya utekelezaji wa majukumu yaliyopo pamoja
na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikakati ya Caritas katika nchi husika.
Wajumbe
walionesha masikitiko yao makubwa kutokana na uwajibikaji wa "Caritas Africa" katika
kuzisaidia nchi wanachama. Kati ya sababu zilizotolewa ni pamoja na ukata na ukosefu
wa rasilimali fedha; baadhi ya viongozi wa Caritas katika nchi husika kutowajibika
barabara kwa kuwa wakweli na wa wazi katika matumizi ya fedha za misaada pamoja na
ukweli kuwa rasilimali iliyopo ni kidogo, ikilinganishwa na mahitaji makubwa yanayotolewa
na nchi wanachama wa "Caritas Africa". Nchi na wafadhili mbali mbali wa "Caritas Africa"
wamepunguza msaada wao kwa kiasi kikubwa Barani Afrika kutokana na athari za myumbo
wa uchumi kimataifa.
Pamoja na mapungufu haya, wajumbe wameamua kuimarisha
mawasiliano, maamuzi, uwajibikaji pamoja na kuonesha thamani ya fedha halisi inayotakiwa
katika kukabiliana na majanga. "Caritas Africa" inazihamasisha nchi wanachama kuchangia
kwa hali na mali katika kupambana na majanga mbali mbali badala ya mtindo wa sasa
kusubiri msaada kutoka kwa nchi na wafadhili mbali mbali.
Barani Afrika kuna
nchi ambazo bado zinahitaji masaada wa dharura ili kuwasaidia watu waliolazimika kuyakimbikia
makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao. Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali,
Niger, Chad, Cameroon na Nigeria ni kati ya nchi ambazo zinakabiliwa na mashambulizi
ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram. Namibia kwa sasa inakabiliwa na
ukame wa muda mrefu ambao unahitaji msaada wa dharura. DRC licha ya vita, Caritas
inaendelea kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi wanaorudi nchini humo. Sudan ya Kusini
ni kati ya nchi ambazo pia zinahitaji msaada wa dharura.
Wajumbe wa "Caritas
Africa" wanaendelea kuhamasishwa kuhakikisha kwamba, wanashirikiana wao kwa wao pamoja
na kujenga mtandao mkubwa zaidi wa mahusiano na mashirika ya misaada, ili kuwasaidia
watu wanaohitaji msaada wa dharura.