Uchaguzi mkuu nchini Nigeria mwaka 2015 unaweza kusababisha majanga!
Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema
kwamba, mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015 unaweza
kuandamwa na matukio ya umwagaji damu kwa watu wasiokuwa na hatia kutokana na watu
kupania kushika madaraka kwa udi na uvumba! Inasikitisha kuona kwamba, viongozi wa
kisiasa wamesahau wajibu wa kulinda na kutetea amani, ustawi na maendeleo ya watu
wao, na badala yake wameanza kugombania madaraka.
Askofu mkuu Kaigama ameyasema
haya hivi karibuni wakati wa mkesha wa kuombea amani, umoja na upatanisho wa kitaifa
kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Kikundi cha Boko Haram kuendelea
kukithiri siku hadi siku, kiasi cha kuwakatisha watu tamaa ya kuishi. Mauaji yanaongezeka
na Boko Haram inaendelea kujitanua kwa kuteka na kukalia miji mingi zaidi, mambo yanayoonesha
udhaifu mkubwa wa Serikali katika kupambana na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram,
ambacho kwa sasa kimekuwa nguzo yao kisiasa.
Kanisa Katoliki litaendelea kukemea
na kulaani vitendo vya kigaidi kwani limeathirika vibaya sana kutokana na mashambulizi
yanayofanywa na vikosi hivi. Kuna watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia
usalama wa maisha yao, lakini hata katika shida na mahangaiko haya, Maaskofu wameendelea
kuwa bega kwa bega na waamini wao kwa kuwapatia faraja na matumaini mpaya; wameendelea
kutoa huduma kwa wananchi wote wa Nigeria bila ubaguzi wa kidini au itikadi ya watu.