2014-11-19 09:21:14

"Tunahitaji mbinu mkakati na mipango kazi ili kupambana na baa la njaa na utapiamlo"


Dr. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jumanne tarehe 18 Novemba 2014 amekutana na kuzungumza na watanzania wanaoishi nchini Italia. RealAudioMP3

Amepongeza juhudi zinazofanywa na watanzania katika kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa wanapokuwa ughaibuni kwa kukuza utaifa wao na kuendeleza lugha ya Kiswahili licha ya maendeleo makubwa ya sayansi ya mawasiliano ya jamii, ambayo kwa sasa inawafanya watu wengi kutopenda kushikamana na wengine kwa kujikita katika ubinafsi.

Kwa ufupi amejibu changamoto mbali mbali zilizotolewa na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Italia katika risala iliyosomwa kwa niaba yao na Bwana Kagutta Nsangu Maulidi. Amesema kwamba, Serikali inaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa kufumua mtandao wa kigaidi uliokuwa umeanza kusababisha hofu kubwa miongoni mwa watanzania kutokana na milipuko ya mabomu iliyokuwa inasikika mara kwa mara, mambo ambayo ni mageni sana kwa watanzania walio wengi, Jamii iliyozoea kuishi kwa amani na utulivu. Amewataka watanzania, kuvumiliana, kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana, ili amani na utulivu viendelee kuimarika zaidi na zaidi.

Serikali inaendelea pia kusuluisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji, ili amani na utulivu viweze kurejea tena kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, dhana iliyofafanuliwa kwa kina na mapana na Dr. Titus Malengeya Kamani, Waziri wa maendeleo ya mifugo na uvuvi nchini Tanzania.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Makamu wa Rais ambaye pamoja na ujumbe wake wanashiriki mkutano wa Lishe na Chakula ulioandaliwa na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO mjini Roma amebainisha kwamba, mkutano huu unafanyika takribani baada ya miaka ishirini na miwili, tangu mkutano wa kwanza ulipofanyika. Ni mkutano unaopania pamoja na mambo mengine kubainisha mbinu na mikakati madhubuti ya kupambana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha unakwamisha makuzi ya watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano.

Upatikanaji wa lishe bora utasaidia kupambana na magonjwa yanayosababisha vifo kwa wanawake wajawazito wakati wa kujifungua pamoja na kuimarisha afya za watoto. Wajumbe wa mkutano hawana budi kufanya kazi kwa kushirikiana, ili maamuzi yatakayofikiwa yasaidie kupambana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha.

Hapa kuna haja anasema Makamu wa Rais kuwa na mikakati na mipango kazi ya utekelezaji wa maazimio haya. Ni aibu kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa baa la njaa na utapiamlo kuendelea kuwanyanyasa watu, wakati ambako dunia inaweza kuzalisha chakula cha kutosha, kiasi kwamba, hata kingine kinatupwa kwenye mashimo ya taka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.