2014-11-18 10:17:13

Ndoa mseto na changamoto zake Barani Afrika


Mapadre kutoka Afrika Magharibi, hivi karibuni wamefanya kongamano la kimataifa ambalo pamoja na mambo mengine, limejadili kuhusu ndoa za mseto na changamoto zake katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Mama Kanisa anaendelea kufanya majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kutambua na kuheshimu tunu msingi za maisha ya kiroho kati ya waamini mbali mbali.

Lakini, viongozi wa Kanisa hawana budi kutambua kwamba, wanayo dhamana ya kuwafunda wanandoa watarajiwa kadiri ya Mafundisho na Mapokeo ya Kanisa Katoliki, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia husika.

Umoja wa Mapadre Afrika Magharibi, katika kongamano lao la kimataifa, umeangalia kwa kina na mapana changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya ndoa na familia mseto sanjari na majadiliano ya kidini. Hii ni changamoto kubwa na endelevu kwani waswahili husema mapenzi hayana mipaka wala hayachagui mahali pa kutua ni sawa na kipepeo.

Mapadre wanasema, Familia nyingi Afrika Magharibi zinakabiliwa na umaskini wa hali na kipato; zinakumbana na sera na mikakati inayokumbatia utamaduni wa kifo; utandawazi unaowakoroga na kuwachanganya watu kimaadili; kuna kinzani za kijamii na kisiasa, mambo yanayokosesha amani na utulivu kwa familia nyingi, bila kusahau udini na misimamo mikali ya kiimani. Zote hizi ni changamoto zinazozikumba familia nyingi Afrika Magharibi.

Mapadre katika kongamano lao, wamezitaka Serikali kuhakikisha kwamba, zinasimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kwamba, Kanisa litoe kipaumbele cha kwanza katika majiundo makini ya wanandoa watarajiwa pamoja na kuwasindikiza wale walioamua kufunga ndoa, ili kweli ndoa zao ziweze kudumu na kuwa ni chemchemi ya mapendo, huruma, wema na msamaha wa kweli.

Waamini wanapaswa kuheshimiana na kuthaminiana wakitambua tofauti zao za kidini ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia. Familia zitambue kwamba, watoto wanaowapata ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; wanapaswa kuwapokea na kuwatunza katika kweli za kiimani, kimaadili na utu wema.

Wazazi wajitahidi kuwarithisha watoto wao upendo wa kweli, ili Kanisa liweze kupata familia imara. Maaskofu kadhaa kutoka Afrika Magharibi wameshiriki pia katika kongamano hili, ili kuchochea majitoleo ya Mapadre katika utume wa familia!







All the contents on this site are copyrighted ©.