2014-11-17 09:20:40

Tafuneni Neno la Mungu katika Familia!


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo!! Karibu katika kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani ambapo kwa wakati huu tunaendelea kuzidonoadonoa kwa umbali hati za Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican, ili ujumbe wake uweze kupyaishwa na kutua katika familia zetu na Maisha yetu ya kila siku. Leo tunaitazama hati ya kikatiba inayoitwa DEI VERBUM. RealAudioMP3

Neno Dei Verbum, maana yake, Neno la Mungu. hii ni hati ya kikatiba inayohusu mafunuo ya Kimungu, tunayoyapata kwa namna mbalimbali, na kwa namna ya pekee kabisa tunayapata katika Neno la Mungu. historia inashuhudia kwamba, kwa muda mrefu watu hawakuzoeshwa kusoma na kuyajifunza maandiko matakatifu, na hivyo kutofahamu vema mambo yaliyofunuliwa kwetu kwa njia ya maandiko Matakatifu.

Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican, ulitazama kwa kina sana juu ya Matumizi ya Maandiko Matakatifu katika maisha mazima ya Mkristo. Mtaguso huo, baada ya majadiliano na marekebisho mengi imelirudishia Kanisa lote Maandiko Matakatifu.

Tangu baada ya Mtaguso huo, kwa msaada wa wataalamu mbalimbali wa maandiko matakatifu, taifa la Mungu wamekuwa wakifundishwa kwa dhati juu ya maandiko Matakatifu. Waseminari na watawa pia wamefundishwa sana Neno la Mungu, na hata walei, japo siyo wote, wamekuwa na ujasiri wa kuyasoma na kuyajifunza maandiko matakatifu. Ndiyo maana katika harakati za Uinjilishaji wa kina, kuna majimbo ambayo yana vikundi vinayoitwa Utume wa Ki-biblia. Hiyo yote ni juhudi ya kufikisha Ufunuo huo wa Kimungu katika maisha ya watu. Na Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo pia, zimeweka Neno la Mungu kama ndiyo Msingi au kiini cha kutaniko na Muungano wao kama Msingi wa Kanisa.

Sura ya kwanza inahusu ufunuo wa Mungu. Sura hii inatueleza uhalisia wa U-historia wa Biblia. Hatuwezi kuelewa Biblia mbali na historia ya wokovu. Ni kitabu kilichoandikwa kutokana na Mafunuo ya Mungu ya hatua kwa hatua katika mazingira mbalimbali na nyakati mbalimbali kwa watu mbalimbali na kwa namna ya pekee kwa njia ya Taifa Teule.

Sura ya pili inafundisha jinsi ufunuo huo uliokamilika kwa njia ya Kristo Yesu na jinsi unavyotufikia sisi kwa njia ya Mapokeo ya Mitume na Maandiko yaliyokwishwa kuwapo. Kwa ujumla wake yanaitwa hazina takatifu ya Neno la Mungu. Hazina hiyo imekabidhiwa kwa Kanisa. Na kwa njia ya Mamlaka fundishi ya Kanisa, Kanisa linaweza kuifundisha, kuifafanua na kuitunza vema ili vizazi vyote vineemeke kwa hazina hii takatifu. Ndiyo maana katika Mafundisho yetu mambo haya matatu yameungana bar’abara: Mapokeo Matakatifu, Maandiko Matakatifu na Mamlaka Fundishi ya Kanisa.

Sura ya tatu inatueleza jinsi Roho Mtakatifu alivyowavuvia waandishi wa Neno la Mungu. Hao walifanya kazi kama waandishi wowote, lakini vitabu vilivyopatikana vinafundisha tu kwa hakika pasipo kosa ule ukweli ambao Mungu alitaka uandikwe kwa ajili ya wokovu wetu. Hivyo Biblia mwandishi wake hasa ni Mungu, lakini yeye alijieleza kwa njia ya wanadamu tena kwa namna ya kibinadamu. Basi, tukitaka kumuelewa tunapaswa kuelewa kwanza waandishi walitaka kusema nini tukizingatia pia namna ya uandishi walioutumia katika mazingira na tamaduni zao.

Mtume Paulo anathibitisha ukweli na uzito wa Neno hilo la Mungu, anapomwandikia Timoteo kusema “Maandiko yote matakatifu yameandikwa kwa Uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundisha ukweli, kuonya, kusahihisha makosa na kuwaongoza watu waishi maisha adili (Rej.2Tim.3:16).

Mpendwa msikilizaji, neno hilo, linapiga hodi katika Kanisa letu la nyumbani. Nasi kama familia tunapenda familia yetu isimame na iongozwe kwa Neno la Mungu. Neno la Mungu ni Mungu mwenyewe. Nguvu ya Neno la Mungu inasaidia sana kuchangia amani na usitawi wa familia inayomcha Mungu.

Mtume Paulo anatukumbusha vizuri sana juu ya machache tunayoweza kuyapata katika maandiko matakatifu. Yapo maadilisho ya kimaadili kwa ajili ya maisha ya kila siku. Yapo maimarisho ya kiimani, yapo pia maangalisho mbalimbali. Hayo yote yanalenga kutujenga sisi kama watu kamili, kimwili, kiroho na kijamii pia. Na tutakubali ukweli kwamba, neno la Mungu ni fumbo. Kila unaposoma maandiko Matakatifu kwa Imani, ni Mungu mwenyewe anaongea dakika hiyo mahali hapo na wewe msomaji. Haongei nawe katika uzamani. Ndiyo maana wakati mwingine, unaweza kusoma neno na kujikuta kinachosemwa kinakuhusu kwa asilimia zote.

Utajiri wa maandiko matakatifu ni wa ajabu, kuna mambo yanayowahusu wazazi, yanayowahusu watoto katika familia, yanayohusu kutimiza wajibu katika maisha yetu ya kila siku, yanayohusu uadilifu katika maisha ya kila siku, na mambo mengine kama hayo, hayo yote yanalenga katika kutujenga kila mmoja binafsi na kama familia kutujenga kwa pamoja.

Tunapotafakari makala hii, tunapeleka rai ya pekee sana katika familia, tupende kuyasoma na kuyajifunza maandiko Matakatifu. Na pia ikiwezekana, kila familia iwe na kifungu cha Andiko takatifu kinachoongoza familia, kama Kauli mbiu kwa familia nzima, ili daima wanafamilia tukumbushwe juu ya uwepo na wito wa Mungu kati yetu. Hata wewe mtu binafsi, uwe na kauli mbiu ya maisha yako, inayosimama katika Biblia Takatifu.

Katika familia zetu, hakika tungekuwa na ujasiri wa kuyasoma maandiko matakatifu, tungepunguza kelele kwa kiasi kikubwa sana. Tungepunguza vikao vingi visivyokuwa na suluhu. Dira ya maisha mazima ya Mkristo yanapatikana katika mafunuo hayo ya Kimungu. Mtume Paulo anaendelea kutuhimiza akisema “tumia wakati wako na juhudi yako katika kusoma hadharani maandiko matakatifu, kuhubiri na kufundisha” (rej.1Tim 4:13).

Hakika, neno la Mungu, linatufundisha, linatukumbusha, linatuimarisha, linatufariji, linatuonya, linatutia moyo, linatupondaponda na kutukata kama upanga wenye makali kuwili ili tuwe watu wazuri, linatuunganisha, linatuinua, linatukinga, linatupatia hekima na busara, linatupa ujasiri, linatutahadharisha; na zaidi ya yote, neno la Mungu ni nuru ya kutuangaza na kutuongoza tupite na tufike salama.

Tukihimizwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican Mintarafu Maandiko Matakatifu, tunakutakia Usomaji mwema wa Biblia Takatifu, na kukiheshimu Kitabu hicho kitakatifu kwa kukitunza kwa stahiki yake.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.