2014-11-17 12:17:27

Papa Francisko anatarajiwa kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya VIII ya Familia Duniani, 2015 huko Philadelfia, USA.


Roho Mtakatifu amemkirimia kila mwamini karama tofauti ili kukamilishana, kwa ajili ya mafao ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa pamoja na kuendeleza maelewano na utulivu yanayojikita katika kazi ya Uumbaji, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhusika mkuu anayewezesha utulivu kupatikana.

Mkamilishano huu ndio msingi thabiti kati ya Bwana na Bibi katika maisha ya ndoa na familia, mahali pa kwanza kabisa ambapo mwanadamu anapata fursa ya kutambua karama za mtu binafsi na zile za jirani yake na hivyo kuanza kujikita katika sanaa ya kuishi karama hizi kwa pamoja. Familia ni mahali ambapo watu wengi wanapata fursa ya kujifunza tunu msingi za maisha pamoja na kumwilisha karama mbali mbali katika mshikamano wa upendo.

Familia pia ni mahali pa kinzani kati ya ubinafsi na mshikamano; kati akili na hulka; kati ya malengo mpito na malengo ya muda mrefu. Familia ni mahali ambapo kinzani hizi zinaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, kwa kuzingatia mkamilishano kati ya Bwana na Bibi, kila mtu akijitahidi kuchangia katika kukuza na kudumisha ndoa pamoja na malezi ya watoto.

Huu ni mchango uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 17 Novemba 2014 wakati alipokuwa anashiriki katika Kongamano lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, kuhusu dhana ya Mkamilishano kati ya Bwana na Bibi, kila mtu akichnagia kutoka katika hazina ya utajiri wake, uzuri na karama.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyakati hizi, Familia inakumbana na changamoto nyingi, kwani watu wanaishi katika utamaduni wa mambo mpito, kiasi kwamba, watu hawaoni tena ile thamani ya maisha ya ndoa; wakati mwingine kwa kupindisha kanuni maadili kwa kisingizio cha uhuru wa mtu binafsi, lakini kimsingi hizi ni dalili za kumong'onyoka kwa tunu msingi za maisha ya kiroho. Kushuka kwa utamaduni wa watu kufunga ndoa ni matokeo pia ya umaskini, hali inayopelekea watu wengi kuteseka.

Kinzani za Familia zimepekea kuibuka kwa tatizo kubwa la Ikolojia ya binadamu, kwani hata mazingira ya maisha ya ndoa na familia yanapaswa kulindwa na kudumishwa, ingawa pengine hata Kanisa limechelewa kuiona changamoto hii, mwaliko wa kuibua mbinu mkakati kwa ajili ya kuendeleza utamaduni wa watu kufunga ndoa, ili kujenga jamii inayosimikwa katika msingi thabiti wa mapendo ya dhati kati ya Bwana na Bibi, ili kuunda mazingira ya malezi na makuzi kwa watoto wao, ndio maana Kanisa linahimiza umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa.

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe hawa katika kongamano hili kuendelea kujadili kwa kina na mapana kuhusu umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa kama kielelezo cha mshikamano, uaminifu na mapendo kamili yanayobubujika kutoka katika moyo wa binadamu. Vijana wafundwe kutambua umuhimu wa Ndoa, ili waweze kutafuta upendo wa dhati na unaodumu, kwa kutambua kwamba, familia inazama katika masuala ya kijamii na kitamaduni na wala si nadharia inayoelea juu ya ombwe! Familia ina nguvu inayojitosheleza yenyewe!

Baba Mtakatifu anawahamisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kulinda na kudumisha mahusiano ya upendo kati ya Bwana na Bibi, kwa ajili ya mafao ya wengi, yanayojikita katika uzuri wa watu, familia, jumuiya na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anasema, panapomajaliwa, kunako mwezi Septemba 2015 atakwenda huko Philadelphia, Marekani, ili kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Nane ya Familia Duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.