Familia ni madhabahu ya Injili ya Uhai inapaswa kudumishwa na kuendelezwa!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 17 Novemba 2014 amekutana na kuzungumza
Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia linalofanya hija yake ya kitume mjini Vatican kwa
kuwatakia kheri na baraka katika kipindi hiki cha sala na tafakari ya kina, ili kujenga
na kuimarisha mshikamano na udugu, ili kuweza kupata mavuno mengi kadiri ya Roho Mtakatifu
anavyowakirimia.
Imani, mapendo na matumaini miongoni mwa wananchi wa Zambia
ni matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu iliyofanywa na Wamissionari hata kama wakati
fulani kazi hii ilikabiliana na kinzani pamoja na changamoto kubwa za kitamaduni,
lakini imani ikaendelea kukua na kuota mizizi katika maisha ya wananchi wa Zambia,
kiasi kwamba, tunu msingi za maisha ya Kikristo zimesaidia kuleta mabadiliko miongoni
mwa wananchi wa Zambia, hasa katika sekta ya afya, elimu na Parokia zinazoendelea
kuibuka kwa wingi nchini humo. Kuna ongezeko kubwa la waamini walei pamoja na miito
ya kipadre na kitawa, neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Zambia inaendelea
kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha, hasa kutokana na ongezeko la
umaskini, hali ambayo inazifanya familia nyingi kutafuta njia za mkato; mambo ambayo
wakati mwingine yanahatarisha imani na matokeo yake ni watu kukata tamaa. Baba Mtakatifu
anasema, Familia inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwani ni msingi wa Jamii, mahali
ambapo watu wanajifunza kuishi kwa pamoja, licha ya tofauti zao msingi na kwamba ni
mahali pa kurithisha imani, dhamana inayotekelezwa na wazazi. Familia ni madhabahu
ya Injili ya Uhai, inayopaswa kudumishwa na kuendelezwa.
Baba Mtakatifu anawataka
viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Zambia kuhakikisha kwamba, wanajifunga kibwebwe
kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, kwa kutoa katekesi ya kina,
ili watu wafahamu ukweli na imani yao kwa kina, ili waweze kulinda na kuitetea dhidi
ya mashambulizi yanayoendelea kujitokeza.
Wanandoa wadumishe uaminifu na mapendo
ya ndoa, wasaidie majiundo ya kina kwa watoto wao sanjari na kudumisha tunu msingi
za maisha ya ndoa na familia yanayojikita katika Mafundisho tanzu ya Kanisa na kumwilishwa
katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Zambia.
Viongozi wa Kanisa waendelee
kuwa karibu zaidi na vijana katika malezi na makuzi yao, ili waweze kuwa na utambulisho
makini, tayari kushiriki katika kazi ya uumbaji kwa kujikita katika wito wa ndoa au
Daraja takatifu au maisha ya kitawa kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Vijana wafundwe
kuchuchumilia usafi wa moyo pamoja na kukuza ushirikiano miongoni mwa utume wa vijana
nchini Zambia, ili wote waweze kujisikia kuwa wako ndani ya Familia ambayo kimsingi
ni Kanisa dogo la nyumbani.
Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa nchini
Zambia kuhakikisha kwamba, wanawasaidia: maskini, wanyonge na wagonjwa, hasa wale
wa Ukimwi, kwani hawa wana nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Watangaziwe
Neno la Mungu, wapewe Sakramenti za Kanisa na kusindikizwa katika hija ya imani yao,
ili kufikia ukamilifu.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu Katoliki
Zambia kuwa karibu na wasaidizi wao wao katika maisha na kazi za Kanisa, kwa kuwaonesha
ukarimu na upendo wa kibaba; kwa kuwasaidia katika mahitaji yao msingi na kuwasaidia,
ili wasimezwe na malimwengu, kwa kuwapatia mambo muhimu ya maisha. Maaskofu waendeleze
hazina kubwa ya maisha ya kitawa katika majimbo yao, ili vijana wengi waweze kujisadaka
kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake bila ya mioyo yao kugawanyika.
Baba Mtakatifu
Francisko amemkumbuka kwa namna ya pekee, Marehemu Rais MIchael Sata aliyefariki dunia
hivi karibuni, kwa kuwataka viongozi wa Kanisa kuendelea kushirikiana na viongozi
wa Serikali kwa ajili ya kutafuta na kudumisha mafao ya wengi; kutoa ushuhuda wa kinabii
kwa kuwatetea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; daima wakiwa wameungana
na kushikamana na Familia ya Mungu nchini Zambia, huku wakishirikishana matendo ya
huruma.
Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa Maaskofu nchini Zambia kuendeleza
mchakato wa Utamadunisho, ili kuweza kusafisha mila na tamaduni zinazosigana na Injili
ya Kristo, ili Watu wa Mungu waweze kupata zawadi ya Injili itakayowaonjesha furaha
na huruma, huku wakijitahidi kuishi kadiri ya changamoto za Kiinjili, ili kushiriki
katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki na amani.
Maaskofu
wanakumbushwa kwamba, wao ni watenda kazi katika shamba la Bwana, dhamana inayohitaji
sadaka binafsi, uvumilivu na upendo unaofumbatwa katika imani na sadaka iliyotolewa
na watangulizi wao, ili kuweza kuliimarisha Kanisa nchini Zambia.