2014-11-15 09:15:16

Misale ya Altare kwa lugha ya Kiswahili yaanza kushughulikiwa!


Tume za Liturujia kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kenya na Tanzania, hivi karibuni zimekutana Nairobi, ili kupanga mkakati utakaoziwezesha tume hizi kutafsiri Misale ya Altare kutoka katika lugha ya Kilatini kwenda lugha ya Kiswahili, kwa ajili ya matumizi ya waamini wanaozungumza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki.

Mradi huu, utawashirikisha wadau wengine kama vile, Idara ya shughuli za kichungaji ya AMECEA na Shirika la Uchapaji la Mabinti wa Mtakatifu Paulo. Misale ya Altare inayotumika kwa sasa ni ile iliyochapishwa kunako mwaka 1969 na Mwaka 1975. Kwa sasa anasema Askofu Salutaris Melchior Libena, Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwamba, kuna mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Kanisa kuhusiana na Misale ya Altare yanayopaswa kurekebishwa kadiri ya tasfiri ya lugha ya Kilatini.

Askofu Dominic Kimengich, Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anasema, nchi hizi mbili, yaani Kenya na Tanzania zinatumia Kiswahili kama lugha ya taifa, kumbe, wanaweza kushirikiana ili kufanya tasfiri ya Misale ya Altare, kama ilivyoshauriwa wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA wakati wa mkutano wake wa kumi na nane, ulioadhimishwa huko Lilongwe, Malawi.

Wadau kwa pamoja, wameandaa mpango kazi, utakaonyambulishwa wakati wa mkutano mwingine unaotarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam, Mwezi, Desemba 2014. Huu utakuwa ni mkutano utakaowashirikisha, wajumbe watakaopewa dhamana ya kutafsiri vitabu hivi kutoka katika lugha ya Kilatini kwenda katika lugha ya Kiswahili.

Inatarajiwa kwamba, tafsiri rasmi ya Misale ya Altare kwa lugha ya Kiswahili inaweza kupatikana kati ya mwezi Mei na Juni 2015 na Muswada wake kuhakikiwa na Mabaraza ya Maaskofu mwezi Septemba 2015, kabla ya kutumwa mjini Vatican kwa ajili ya kuidhinishwa rasmi na Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa.









All the contents on this site are copyrighted ©.