2014-11-03 07:15:20

Mwanadamu anajifanya kuwa ni "mungu mdogo" chanzo cha majanga mengi duniani!


Mwanadamu anayejikuza na kujifanya kuwa ni “mungu mdogo” ni hatari kwa mazingira na maisha ya wanadamu wanaolalama kila siku kutafuta chakula na mahitaji yao msingi; ni hatari kwa watoto wanaoendelea kufa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Binadamu wa leo ana uwezo mkubwa wa kuharibu kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemdhaminisha mwanadamu.

Hii ni sehemu ya mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe Mosi, Novemba 2014 kwenye Makaburi ya mji wa Roma, wakati alipokuwa anasali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea marehemu wote, siku ambayo kimsingi inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba. Baba Mtakatifu ameelezea machungu yake kwa kusema kwamba, binadamu amekuwa ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira, maisha, tamaduni, tunu msingi za maisha, kiasi hata cha kukosa matumaini.

Kutokana na mwelekeo kama huu, mwanadamu hana budi kuomba nguvu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, nguvu ambazo zinafumbata upendo ili kudhibiti mashindano haya yanayoendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya mwanadamu. Mwanadamu amekuwa ni sababu kubwa ya uharibifu wa kazi ya Uumbaji, ambayo ilipaswa kulindwa na kutunzwa, ili iweze kukua na kuzaa matunda yanayokusudiwa. Baba Mtakatifu amesikitishwa na uharibifu wa vita uliofanywa kunako mwaka 1943 na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa. Lakini anasema, vita inayoendelea kwa sasa sehemu mbali mbali za dunia ina madhara makubwa kwa watu na mali zao.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, binadamu anajifanya kuwa ni “mungu mdogo” na mfalme wa yote, kiasi cha kuendeleza vita inayopandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo na hali ya kutojali, hata maisha ya mwanadamu ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hivi ndivyo wanavyotendewa watoto, wazee na vijana wasikuwa na fursa za ajira; hiki ni kielelezo cha utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu.

Baba Mtakatifu anawakumbuka kwa namna ya pekee maskini, watu wasiokuwa na makazi, wagonjwa na wenye njaa; wote hawa ni matokeo ya binadamu aliyejifanya kuwa ni “mungu” mdogo, anayemiliki na kutawala kazi ya Uumbaji; uzuri ambao Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu. Waathirika wakuu ni maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ambao utu na heshima yao havithaminiwi hata kidogo. Huu ni umati wa watu ambao wako mbele ya Mwenyezi Mungu wakimlilia ili kupata wokovu, amani na mahitaji yao msingi. Ni watu wanaotafuta fursa za ajira, ili kulinda na kudumisha utu na heshima yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema katika mahubiri yake wakati wa kuwakumbuka Marehemu wote kwamba, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya matumaini kwa watu wake, hata katika shida na mahangaiko bado anawajali na kuwathamini. Ni mwingi wa huruma na mapendo na kwamba, hiki ndicho kielelezo makini cha Kanisa, tayari kusonga mbele katika safari ya kukutana na Mwenyezi Mungu uso kwa uso baada ya maisha ya hapa duniani.

Ni changamoto na mwaliko kwa waamini kujivika silaha za mafundisho ya Heri za Mlimani, zitakaokoa mazingira, kanuni maadili, historia na familia ya mwanadamu. Ni hija inayojipambanua hata kwa mateso na madhulumu, mateso na mahangaiko ya watu, lakini daima wakiwa na tumaini la kukutana na Mwenyezi Mungu, ili waweze kushiriki katika utakatifu wake.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili awajalie neema na ujasiri wa kuondokana na mambo ambayo yanasababisha uharibifu, utepetevu wa maadili, ubaguzi kwa kujikita katika umoja na amani, huku wakitembea katika hija ya matumaini.

Wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, kuliwekwa Masalia ya Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II waliotangazwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko hapa mjini Vatican.

Mahubiri haya yamehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.