2014-10-31 07:30:44

Sinodi imeliwezesha Kanisa kuona na kusikiliza kwa dhati!


Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia ni kielelezo cha mchakato wa Mama Kanisa kutaka kusikiliza kwa dhati kabisa furaha, matatizo na changamoto ambazo familia zinakabiliana nazo katika ulimwengu mamboleo. Ni maneno ya Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu alipokutana na kuzungumza na Wabunge kutoka Uingereza, waliomtembelea mjini Vatican Alhamisi, tarehe 30 Oktoba 2014.

Katika mazungumzo yake, amewashirikisha wabunge hao mambo makuu yaliyojitokeza wakati wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia pamoja na changamoto zilizoibuliwa na Mababa wa Sinodi. Kadiri ya maelezo yaliyokuwa yanatolewa na baadhi ya vyombo vya habari inaweza kudhaniwa kwamba, maadhimisho ya Sinodi, yalikuwa ni "patashika nguo kuchanika", lakini, kimsingi maadhimisho haya yalikuwa ni mang'amuzi makubwa kwa Mama Kanisa kutembea kwa pamoja na kusikiliza kwa dhati changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa kuhusiana na maisha ya ndoa na familia.

Mafanikio makubwa yaliyojitokeza katika maadhimisho haya ni utambuzi wa umuhimu wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, Kristo Mfufuka amewajalia wafuasi wake zawadi ya Roho Mtakatifu, ili kuweza kushiriki kwa ukamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa litaendelea kujikita katika Mafundisho yake tanzu, Maandiko Matakatifu na Mapokeo, pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kuweza kukabiliana na changamoto za nyakati hizi.

Kardinali Baldiserri anasema, kati ya changamoto kubwa kwa sasa ni waamini kutalikiana, mwelekeo wa ndoa za watu wa jinsia moja na ndoa za wake wengi. Changamoto hizi zimejadiliwa kwa kina na mapana katika maswali dodoso yaliyotumwa kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, jambo ambalo limewasaidia Mababa wa Sinodi kufahamu ukweli wa maisha ya ndoa na familia katika undani wake.

Kuna baadhi ya watu wameshutumu msimamo na ukweli wa Mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia na baadhi yao wamelishauri Kanisa kufanya maamuzi magumu kwa kuzingatia changamoto za watu wa nyakati hizi. Kardinali Baldisseri anasema, jambo la kufurahisha ni kuona kwamba, waamini wanaifahamu Injili na kanuni maadili katika maisha ya ndoa na familia, mambo ambayo hayawezi kuwekwa kando kwani ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Viongozi wa Kanisa wamepewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanatekeleza utume wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu kadiri ya mafundisho ya Mama Kanisa.

Mababa wa Sinodi katika ukweli na uwazi; kwa moyo wa unyenyekevu na hekima, wameshirikishana mambo msingi ambayo yanaweza kulisaidia Kanisa kuandaa mikakati ya kichungaji kwa ajili ya watu wa ndoa na familia, ili Mama Kanisa aendelee kutangaza Injili ya Familia kwa Watu wa Mataifa. Sinodi ilipania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, inafafanua Mafundisho ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia mintarafu mwelekeo wa kimissionari na kichungaji.

Kanisa linatambua kwamba ni chombo cha wokovu, huruma na upendo, lina dhamana ya kuwapokea na kuwakumbatia wote, watakatifu na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Mababa wa Sinodi wameshirikisha kuhusu uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia; utu na heshima ya maisha ya ndoa; mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake.

Dhamana ya Mama Kanisa ni kuendelea kutangaza Injili ya Familia kwa kuzingatia: ukweli na uwazi, kwa unyenyekevu na busara, huku akiwasindikiza wanafamilia wanaogelea katika shida na mahangaiko mbali mbali ya maisha. Kwa kutambua haya yote, hapa Mama Kanisa anataka kupiga hatua nyingine tena kwa kuwaalika watoto wake kutubu na kumwongokea Mungu; daima wakijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao; kwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa.

Kardinali Baldisseri anasema, huu ndio ukweli wa mchakato wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia, kama walivyoonesha Mababa wa Sinodi na Baba Mtakatifu Francisko akaweka mkazo wa pekee kama mhimili wa umoja na mshikamano wa Kanisa, changamoto kwa waamini kukumbatia kweli za Kiinjili.

Viongozi wa Kanisa wataendelea kuwaganga na kuwaponya waamini wanaokabiliana na madonda makubwa katika maisha ya ndoa na familia, kwa kutumia kweli za Kiinjili na Huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Mada zilizojadiliwa na Mababa wa Sinodi zilikuwa zinagusa maisha ya watu wengi ndiyo maana vyombo vya habari vilikuwa vinafuatilia kwa makini mchakato wa maadhimisho ya Sinodi.

Mababa wa Sinodi wamejitahidi kujikita katika mambo msingi ya maisha ya ndoa na familia; kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu; mambo msingi ambayo yanapaswa kutolewa ushuhuda na Wakatoliki katika hija ya maisha yao ya kila siku!







All the contents on this site are copyrighted ©.