Mungu amewekeza siri ya upendo katika Fumbo la KIFO!
Kifo ni kitendawili ambacho binadamu ameshindwa kabisa kukitegua. Anabaki kuhoji na
kujihoji bila kupata jibu la kwa nini anakufa. Mbele ya kifo binadamu anabaki kutoa
visingizio vya kujitetea na kulaumu, hatimaye anakiona kifo kuwa mwiko.
Zamani mwiko
ulikuwa masuala ya „mapenzi”, kumbe kifo na misiba hakikuwa kitu cha kuogopa sana.
Lakini sasa ni kinyume, mambo ya mapenzi yamegeuka kuwa kitu cha kawaida kabisa isipokuwa
kifo kimekuwa kiboko chetu.
Watu tunakiogopa na pengine hatutaki hata kukisikia.
Tunapolazimika kwenda msiba basi tunawaachia wengine walipambe jeneza maua, nasi tukisubiri
kwenda kutia sahihi kwenye kitabu cha maombolezo na kutoa rambirambi kwenye bahasha
kisha kukaa mbani na jeneza huku tukizungumza chinichini. Sanasana tunajisahaulisha
kwa kuimba nyimbo za maombolezo au kusikiliza nyimbo za Injili. Tunaogopa kabisa kukizungumzia
kifo au walau kukijadili. Mbele ya kifo binadamu tunabaki kulaumiana, kushikana uchawi
na hasa tunamlaumu Mwenyezi Mungu.
Mathalani, kuna baadhi ya wakristu wa kale
hata wa sasa walisali na kuomba msaada kwa Mungu au kwa kupitia watakatifu fulani
kusudi waepushwe na kifo. Sala hizo zinapoacha kupokelewa, binadamu anachukia, na
kumlaumu Mungu. Kristu aliwahi pia kulaumiwa pale alipokataa mwito wa Marta na Maria
walipomwomba aenda kwao kumponyesha kaka yao Lazaro aliyekuwa mgonjwa. Yesu akaenda
huko kwa kuchelewa kusudi siku nne baada ya kifo. Siku ile alipojionesha msibani,
Maria na Marta wakamjia juu na kumlaumu sana. “Bwana ungalikuwapo ndugu yetu asingalikufa”.
Hata katika nafasi hiyo, bado hatutaki kulijibu swali ni sababu gani Yesu alifika
duniani. Je Yesu alifika duniani ili kuendeleza uhai huu wa kibaolojia au kushinda
mauti?
Tukitaka kujua ukweli wa mwenendo mzima wa maisha yetu, hatuna budi
kuangalia pia hatima yake, yaani kuelewa kwamba maisha yetu yana mwanzo (yaani kuzaliwa)
na yana ukamilifu wake. Ama sivyo tutaendelea kukiogopa kifo, nacho kitaendelea kupeta
na kutuogofya zaidi.
Ndugu zangu, tulishukuru Kanisa limetutengea mwezi mzima
wa Novemba tulioishauanza ili tukitafakari kitendawili hiki cha kifo. Asiyetaka kukitafakari
kifo anaonywa na methali ya kiswahili isemayo: “Asiyejua kufa na atazame kaburi.”
Kwa hiyo tunaalikwa pia kwenda makaburi mara nyingi kuwaona wenzetu walioishapambana
na kifo, nao watatusaidia kutafakari vizuri zaidi fumbo hilo la kifo.
Hebu
tujaribu kutafakari kidogo na kupata jibu stahiki juu ya kifo na hatima ya maisha
yetu. Tuanze utafiti wetu na Wayahudi, hasahasa manabii na wanazaburi. Wenzetu walianza
utafiti mpya juu ya kifo wakitegemeza hoja zao juu ya kitu hiki “upendo”. Yaani kama
Mungu aliingia katika mahusiano na binadamu na kufanya naye maagano iwe kwa njia ya
manabii wa aina yoyote ile ni kwa sababu Mungu alimpenda binadamu na hivi akataka
kuwa na mawasiliano naye. Ukimpenda mtu kwa dhati, huwezi ukamwacha tu kienyeji.
Hiyo
ndiyo sheria ya upendo. Kwa hiyo ukisema: “Mungu ninakupenda”, naye akikuambia “Ninakupenda”,
basi upendo huo hauwezi kwisha. Namna hii ya kufikiri, ina nguvu sana katika maisha.
Katika Agano la kale, Mungu anawaambia wayahudi: “Wewe una thamani machoni pangu,
nami ninakupenda” (Isaya). Hapo yaonesha wazi kuwa Mungu anao mradi wa kumpenda kiumbe
chake kwa sababu amemwumba. Kwa hiyo katika Injili, tunaona kuwa katika mradi huo,
Mungu amewekeza katika upendo kwa njia ya udalali ambao ni yeye mwenyewe katika nafsi
ya pili ya Mungu, Yesu Kristu.
Injili ya leo imechukuliwa toka mazungumzo juu
ya chakula cha uzima Ekaristi. Mradi huo wa Mungu umeanishwa kwa neno moja tu “Mapenzi”.
Neno hilo limetamkwa na Yesu karibu mara nne: “sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye
mapenzi yangu”; halafu, “bali niyafanye mapenzi yake aliyenipeleka”; halafu tena “Mapenzi
yake aliyenipeleka ni haya”; na mwisho “Kwa kuwa mapenzi yake baba yangu ni haya”.
Hebu
tumwangalie kwa undani Dalali aliyekabidhiwa kutekeleza mradi wa Mungu kwa wanadamu
anasema: “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje
kamwe”. Hivi ndiyo Mungu anavyomwaminisha Yesu mradi huo wa mapendo kwa binadamu.
Mungu anauaminisha ubinadamu wote kwa Yesu bila masherti. Kwa hiyo ili kuelewa maana
ya kifo na ukombozi toka kifo, yabidi tuingie katika mradi huo wa mahusiano ya upendo
(mapenzi) na Yesu.
Hoja ya msingi ya kuingia katika mahusiano hayo ni ile
anayoisema Yesu mwenyewe, “Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi
yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” Hivi ni dhahiri kwamba Yesu amefika duniani
kama dalali ili kutekeleza mradi wa Mungu, yaani kunadisha na kuendeleza mahusiano
hayo ya upendo. Mungu amemdhamini Kristu mwanae mradi mzima wa upendo. Kama anavyothibitisha
Yesu mwenyewe: “Mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa
nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho.” Hapo ndipo palipojaa uhondo!
Maana yake bila Kristu, hatuwezi kupata jibu sahihi juu ya kifo, jibu linalookoa na
kuelewa mwisho au hatima yetu. Na Yesu aliye mdhamini wa mradi huo hataki kujiangusha
mwenyewe anaposema, “Katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku
ya mwisho” anamaanisha kwamba atatuwapelekesha hao aliokabidhiwa hadi kieleweke.
Kufufuliwa
siku ya mwisho, kadiri ya mwinjili Yohane haimaanishi mwisho wa dunia, bali ni Kalvario,
juu ya msalaba siku ile anaposulibiwa na kufa. Tendo la mwisho la Yesu la upendo ni
pale alipoitoa roho na maisha yake ya kimungu, nguvu ya upendo aliyoitolea yote kabisa
wakati wa uhai wake na kuihitimisha pale msalabani. Siku hiyo ya mwisho anaitoa roho
yake na maisha yale ya milele yanaingia kwenye mahusiano ya daima na Mungu, na maisha
hayo hayana mwisho. Hayo ndiyo mapenzi ya Mungu.
Mradi huo unatekelezeka tu
endapo tutamtambua Mungu katika Kristu: “Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya,
ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua
siku ya mwisho.” Maana yake, upendo huo wa Baba utatekelezeka kwa namna tatu:
kwanza kwa yule “amtazamaye Mwana,” kumbe yatubidi kuona au kutazama. Kuutazama au
kuuona huu mradi wa Mungu na kumtambua Kristu ambaye ndiye mdhamini mkuu wa Mungu.
Halafu yabidi “kumwamini Yesu”, yaani kutoa ushuhudi wa binafsi kwa huyo mdhamini
pekee. Kisha matokeo ya kumtambua na kuishi kama alivyoishi huyo mdhamini yatakuwa
ni “kufufuliwa naye”.
Kwa hiyo katika maisha yetu yatubidi tuyadhihirishe
hayo mahusiano ya mapendo na Mungu kwa njia ya Kristu mdhamini wa mapendo. Kwa wale
wenzetu walioishazaliwa kwa Baba, yaani waliofariki, wameutambua tayari uso wa Yesu
na kumwaminia hivi sasa wamepokea maisha ya kimungu. Kwao hao sisi leo tunawapa ushirikiano
kwa kuwa karibu sana nao, na siyo leo tu bali daima. Kama maisha yao hayakuwa makamilifu,
sisi tuwaombee yaani kuwaonesha upendo, kwani Mungu amewekeza upendo katika Yesu Kristu. Padre
Alcuin Nyirenda, OSB.