Maisha ya wahamiaji na wakimbizi wengi yako mashakani!
Kardinali Antonio Maria Veglio', Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji
kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum anasikitika kusema kwamba,
wahamiaji na wakimbizi wengi watakufa maji pasi na msaada huko baharini kutokana na
uamuzi wa Serikali ya Italia kuacha kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji waliokuwa
hatarini wakati wakijaribu kuvuka bahari kuingia Barani Ulaya. Kuanzia tarehe Mosi,
Novemba, huduma hii inatolewa na Jumuiya ya Ulaya na unajulikana kwa jina la "Triton".
Huduma
ya Triton imekabidhiwa meli sita, ndege mbili na elikopta moja kwa ajili ya huduma
katika Bahari ya Mediterania, changamoto ambayo inapaswa kuvaliwa njuga na nchi wanachama
wa Jumuiya ya Ulaya, bila kutegeana, ili kuokoa maisha ya wahamiaji na wakimbizi wengi
wanaotafuta nafasi ya kuingia Barani Ulaya
Kardinali Veglio' anasema kwamba,
uhamiaji ni tatizo kubwa na lenye changamoto kibao kutokana na utete wake, kwani kuna
makundi makubwa ya watu yanalazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa
maisha yao kutokana na: vita, njaa, umaskini; dhuluma na nyanyaso za kidini na hata
wakati mwingine watu wanakimbia nchi zao kutokana na majanga asilia. Wakimbizi kutoka
Syria, Iraq na Ethiopia wanaendelea kuongezeka siku hadi siku kutokana na hali halisi
ilivyo katika nchi hizi.
Serikali ya Italia ilianza kutoa huduma ya kuokoa
wahamiaji na wakimbizi baharini kunako tarehe 3 Oktoba 2013, wakati dunia iliposhuhudia
watu 368 wakizama na kufa maji baharini. Licha ya jitihada hizi, bado kuna watu zaidi
ya 300 wamefariki maji katika kipindi cha mwaka mzima uliopita, changamoto kwa Jumuiya
ya KImataifa kuonesha moyo wa huruma na mshikamano kwa watu wanaotafuta hifadhi ili
kuokoa maisha yao kutokana na majanga mbali mbali wanayokabiliana nayo.
Wakimbizi
na wahamiaji hawa ni watu ambao wameonja suluba na mateso makali kabla ya kuchukua
maamuzi machungu ya kupanda mashua huku wakifahamu fika kwamba, wanatembea na kifo
machoni pao. Mwelekeo wa nchi mbali mbali za Ulaya kuziba masikio, kufunga macho na
midomo yao ili kutosikiliza kilio na mahangaiko ya wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta
hifadhi ya maisha ni jambo la kusikitisha sana na kwamba, hiki ni kielelezo cha kumong'nyoka
kwa utu na mshikamano kati ya watu. Ni utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko
ya wengine kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.
Wakimbizi na wahamiaji
ni tatizo na changamoto endelevu katika maisha ya mwanadamu, jambo la msingi ni kwa
watu kuelimishwa na kufahamishwa kuhusu changamoto hii ili kuifanyia kazi badala ya
kuwafukuza na kuwataka warejee makwao ambako watakumbana na kifo uso kwa uso!