Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alionesha wasi wasi wake kutokana na kuongezeka
kwa maambukizi ya ugonjwa wa Ebola sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya
pekee Afrika Magharibi ambako kuna watu wengi wanaendelea kuathirika.
Baba
Mtakatifu alionesha kwa kuguswa sana na mahangaiko ya watu hawa na kusema kwamba,
anawakumbuka katika sala zake na kuwashuruku wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja
na watu wanaoendelea kujitolea kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu walioathirika kwa
ugonjwa wa Ebola. Ni watu wanaoonesha ujasiri kwa kuwasaidia wengine.
Baba
Mtakatifu Francisko alitumia fursa hii kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe
kuhakikisha kwamba, ugonjwa wa Ebola unapatiwa ufumbuzi wa kudumu pamoja na kuwaomba
watu kuendelea kuwaombea wale wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana
na ugonjwa wa Ebola.
Kwa upande wake, Bwana Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa anasema kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa jibu makini kama sehemu
ya mchakato wa kupambana na ugonjwa wa Ebola, kwani kwa sasa Ebola linaonekana kuwa
ni janga la kimataifa. Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia juhudi za kutokomeza ugonjwa
huu kutoka katika sura ya dunia. Amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wanaotoa
huduma kwa watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ebola, kwa kuonesha upendo na mshikamano
wa dhati.