2014-10-31 10:54:02

Changamoto za mawasiliano katika ulimwengu wa digitali!


Wakurugenzi wa habari kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 5 Novemba 2014 watakuwa na mkutano utakaojadili pamoja na mambo mengine mawasiliano kama njia ya kukutanisha watu, kati ya ukweli na utekelezaji wake. Ni mkutano unaolenga kupembua kwa kina na mapana mchango wa Baba Mtakatifu Francisko katika vyombo vya mawasiliano ya kijamii, kama sehemu ya mchakato wa kumwilisha imani katika matendo, katika ulimwengu wa digitali.

Wawezeshaji wa mkutano huu ni mabingwa na wataalama wa masuala ya mawasiliano ya jamii kutoka Barani Ulaya, wanaopenda kushirikisha uwezo na mang'amuzi kuhusu mwilingiliano wa watu katika njia ya za mawasiliano katika ulimwengu wa digitali na uwezekano wa watu kukutana katika uhalisia wa maisha. Kwa miaka mingi Kanisa limekuwa ni mdau mkuu wa matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, lakini wajumbe wanapenda kujiuliza swali la msingi, Je, Kanisa limefanikiwa kwa kiasi gani kutumia vyombo vya mawasiliano ya Jamii katika kutangaza kweli za Kiinjili?

Huu ni wakati muafaka wa kufanya tafakari ya kina kuhusu ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko alioutoa kwa Kanisa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Habari Duniani kwa Mwaka 2014. Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii atakuwa ni kati ya washiriki 30 kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya. Mkutano huu unafanyika katika hali ya faragha.







All the contents on this site are copyrighted ©.