Ben Kiko katangulia mbele ya haki! Atambukwa na wengi enzi zake!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia
Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt.
Fenela Mukangara kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mtangazaji na Mwandishi Mkongwe na
Mahiri hapa nchini wa iliyokuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo kwa sasa
ni TBC Taifa, Ben Hamis Kikoromo maarufu kama Ben Kiko.
Ben Kiko amefariki
dunia usiku wa kuamkia tarehe 31 Oktoba, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
(MNH) Jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa akiendelea na matibabu ya figo baada
ya kuhamishiwa hapo akitokea Hospitali ya Jeshi ya Milambo Mkoani Tabora. “Nimeshtushwa,
nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mwanahabari na
Mtangazaji huyu Mahiri ambaye ametoa mchango mkubwa wa kihabari kwa Taifa letu”, amesema
Rais Kikwete akiomboleza msiba wa Ben Hamis Kikoromo.
“Namkumbuka Marehemu
Ben Kiko, enzi za uhai wake, kama Mtangazaji aliyekuwa na mvuto mkubwa kwa wasikilizaji
wake kutokana na namna yake ya kipekee ya kuripoti matukio hususan katika kipindi
kilichojizolea umaarufu mkubwa wakati huo cha MAJIRA kilichokuwa kikirushwa hewani
na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD)”.
Wakati wa vita dhidi ya Nduli Idi Amin
wa Uganda mwaka 1978, Ben Hamis Kikoromo alifanya kazi kubwa kwa Taifa kwani aliweza
kuripoti matukio mbalimbali kutoka katika uwanja wenyewe wa vita, na hivyo kuliwezesha
Taifa na wananchi kwa ujumla kuhabarika vilivyo na matukio yaliyokuwa yakiendelea.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, pokea salamu zangu za Rambirambi kutoka dhati
ya moyo wangu kwa kumpoteza mmoja wa Waandishi na Watangazaji Mahiri katika Tasnia
ya Habari hapa nchini.
Vilevile kupitia kwako, naomba Salamu zangu za Rambirambi
na pole nyingi ziifikie Familia ya Marehemu Ben Hamis Kikoromo kwa kupoteza Kiongozi
na Mhimili Madhubuti wa Familia. Nawaomba Wanafamilia wote, ndugu na Jamaa wa Marehemu
wawe wavumilivu na wenye subira wanapoomboleza kifo cha mpendwa wao huku wakitambua
kuwa yote ni mapenzi yake Mola”, amesema Rais Kikwete.
Amewahakikishia Wanafamilia
kuwa yuko pamoja nao katika muda wote wa maombolezo, na anamuomba Mwenyezi Mungu,
Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Ben Hamis
Kikoromo, Amina.
Aidha Rais Kikwete ametuma Salamu za Rambirambi kwa Wanahabari
kote nchini ambao kwa hakika msiba wa Ben Kiko utakuwa umewagusa kwa karibu. Hata
hivyo amesema kuondoka kwa Ben Kiko kusiwe chanzo cha wao kukata tamaa, bali kifo
chake hakina budi kuwa chachu katika kujituma zaidi, na wawe tayari kuiga yote mazuri
aliyoyafanya Marehemu enzi za uhai wake hapa duniani hususan katika Taaluma ya Uandishi
wa Habari.