Maendeleo ya kweli yazingatie mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili
Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu wa kimaadili kulinda na kutetea haki msingi za watu
mahalia, lakini kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa haki msingi za binadamu na uhuru
wa kweli, ili kuwashirikisha kikamilifu katika mchakato wa maendeleo yanayozingatia
mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Sera na mikakati ya maendeleo haina budi
kuwahusisha watu mahalia, kwa kuheshimu utambulisho na tamaduni zao, bila ubaguzi.
Ni
mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernaditto Auza, Mwakilishi wa kudumu
wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa wakati akichangia mada kwenye mkutano mkuu wa sitini
na tisa wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa uliokuwa unajadili haki msingi za watu mahalia.
Ujumbe wa Vatican unaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali mbali mbali katika
kufutilia mbali ubaguzi kwa kuhakikisha kwamba, watu mahalia wanashiriki kikamilifu
katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya maendeleo yao.
Jumuiya
ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, utamaduni wa watu mahalia unalindwa na
kuendelezwa, kwa kuheshimu tunu msingi za maisha ya watu zinazojikita katika zawadi
ya maisha, utu na ushiriki wa watu katika masuala yanayowagusa kwa karibu zaidi bila
kusahau ibada zao. Katika ulimwengu wa utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia
pamoja na kuibuka kwa miji, tunu hizi msingi zinaweza kubezwa na hatimaye kuwekwa
kando kama “gari bovu”.
Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu, umekazia pamoja
na mambo mengine, umuhimu wa kulinda na kuheshimu utu wa watu mahalia; haki ya kupata
maendeleo ya kweli mintarafu utambulisho na tunu msingi za maisha pamoja na kushirikishwa
katika kufanya na kutekeleza maamuzi mbali mbali. Hapa kuna haja ya kudumisha sheria
zinazojikita katika haki; umiliki wa ardhi na utunzaji bora wa mazingira.