2014-10-30 08:00:15

Dumisheni utulivu, amani na mshikamano wa kitaifa!


Jukwaa la Wakristo nchini Zambia katika taarifa yake linasema, limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Michael Chilufya Sata, kilichotokea mjini London, tarehe 28 Oktoba 2014 na kwamba, linapenda kutuma salam zake za rambi rambi kwa familia, serikali na kwa wananchi wote wa Zambia, hasa katika kipindi hiki cha maombolezo makubwa. Ni kifo ambacho kimetokea punde tu baada ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Uhuru wa Zambia.

Jukwaa la Wakristo Zambia linawataka wananchi wote kuendeleza utulivu, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kutoa heshima zao za dhati kwa Marehemu Rais Michael Chilufya Sata. Wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana katika sala, ili kuombea kipindi hiki cha mabadiliko makubwa katika Serikali na nchi katika ujumla wake. Wananchi wa Zambia wamrudie Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, ili aweze kuwafariji katika kipindi hiki cha majonzi. Kwa namna ya pekee, wanaiombea roho ya Marehemu Rais Sata, ipumzike kwa amani. Amina.







All the contents on this site are copyrighted ©.