Tunakuletea habari njema ya furaha tunapotafakari pamoja Neno la Mungu katika sherehe
ya Watakatifu wote. Mama Kanisa akitaka kuhitimisha mwaka wa Kanisa kwa furaha anaona
ni vema awaoneshe watoto wake lengo la maisha ya kikristu yaani ni kuelekea maisha
ya utakatifu, maisha ya ya milele mbinguni.
Kumbe, Mama
Kanisa amependa kila tarehe 1Novemba ya kila mwaka, sherehe hii iadhimishwe katika
Kanisa zima la ulimwengu. Adhimisho hili ni mwaliko kwetu kuchuchumalia maisha yanayotimiza
mapenzi ya Mungu, maisha ya ufufuko ambayo Mtume Paulo anatuambia daima akisema basi
mkishafufuliwa mkayatazame yaliyo ya juu!
Mpendwa, yafaa kutambua watakatifu
ni akina nani? Watakatifu ni wale wanaokaa na Mungu katika kiti chake cha enzi kadiri
tusomavyo katika kitabu cha Ufunuo. Ni marafiki wa kweli au tunaweza kusema ni marafiki
wa dhati au wa kina. Katika lugha yangu ya kihaya Watakatifu tunaweza kuwalinganisha
na “Abatahanju” yaani wale ambao huingia ndani ya nyumba mpaka sebule ya nyuma na
hata jikoni.
Ni wale ambao hula chakula pamoja na mkuu wa familia, na hivi
wanafurahi pamoja na Mungu Baba huko mbinguni. Ni wale ambao Injili ilikuwa chakula
chao cha kila siku walipokuwa duniani na walijikabidhi katika mikono ya Mungu na kuwa
mali yake. Ni wale walioishi heri nane mafundisho ya Kristu aliyoyatoa pale mlimani.
Ni wale ambao walitunza neema ya UTAKASO waliyoipokea wakati wa Ubatizo.
Ni
wale ambao walimpenda Mungu kwa moyo wao wote, kwa akili yao yote na kwa nguvu zao
zote na kisha wakampenda jirani aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni wale ambao
katika ubinadamu wao walikubali mateso wakitambua na kujua siri ya furaha watakayoipata
milele. Sasa wanafurahia matunda ya msalaba wa Kristu. Kwa kifupi ni wale walioshika
vema amri kuu ya mapendo.
Ili basi nasi tuweze kufikia hali hiyo iliyo heri
na furaha upeo, somo la kwanza linaweka mwaliko kwa watu wote kuwa, ili mmoja aweze
kupokea heri za milele yaani utakatifu, ni lazima kufua mavazi katika Damu ya Mwanakondoo.
Ni lazima kukinywea kikombe kimoja cha Damu Takatifu iliyo thamani ya wokovu kwa wote.
Ndiyo kusema ni kuishi kwa kutimiza mapenzi ya Mungu.
Kwa kufua mavazi katika
Damu ya Mwanakondoo kunamwondoa mtu katika dhiki ya dhambi na dhiki ya upungufu wa
upendo mkamilifu. Mmoja ananyakuliwa toka taabu ya ulimwengu geugeu na kuvikwa mavazi
meupe ndiyo utakaso mkamilifu unaowezesha kuimba baraka na utukufu na hekima na shukrani
na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina. Huu ni
wimbo wa sifa kwa Mungu ambao unaweza kuimbwa na walio wake, ndiyo watakatifu.
Katika
Injili ya Mathayo tunapata mafundisho ya Yesu mlimani yaani Heri Nane. Bwana anaonesha
njia ya kufikia utakatifu, njia ya kuishi mapenzi ya Mungu. Anaainisha namna ya kufika
mbinguni, akisema, wanaheri wale walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni
wao. Wanaheri wenye upole maana watairithi nchi. Anazidi kukazia utakaso wa roho akisema
heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu. Hizi ni baadhi ya heri nane za mlimani
njia kamilifu ya kufikia utakatifu.
Kwa kuzitafakari heri nane tunaweza kusema
mambo makuu mawili ni lazima katika kufikia utakatifu. Jambo la kwanza ni kujitenga
na chachu ya ulimwengu. Kumbuka Bwana anasali na kusema tuko ulimwenguni lakini
sisi si wa ulimwengu. Hii yamaanisha kujitenga na kile kinachopingana na injili ya
Bwana, na hivi kuwa maskini wa roho. Kumbe mkristu anapaswa ajisikie daima kinyume
na mawimbi ya ulimwengu yanayopingana na Injili. Jambo la pili ni lile la kupokea
kikombe cha mateso daima na kulitangaza jina la Bwana.
Mateso haya hugeuka
na kuwa furaha katika maisha ya mkristu sasa anapoishi na baadaye. Mtakatifu lazima
aoneshe sura ya Kristu mteswa na mwenye furaha kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu.
Mtakatifu ni lazima amwilishe Heri Nane katika maisha yake na hivi zingae daima na
kuwa kielelezo cha maisha ya upendo.
Mpendwa hiyo ndiyo habari ya upendo mkamilifu
utokao kwa Mungu kwa ajili ya watu wote, na sasa unaalikwa kushiriki zawadi hii ya
upendo bila kuchelewa tunapowashangilia watakatifu wa Mbinguni. Tumsifu Yesu Kristu.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.