2014-10-29 12:18:04

Hija ya kichungaji ya Papa Francisko nchini Uturuki, inaonesha matumaini na ujasiri!


Kwa mara ya kwanza Mwenyeheri Paulo VI alitembelea nchini Uturuki kunako mwaka 1967 na Mtakatifu Yohane Paulo II akafanya hija ya kichungaji nchini humo kunako mwaka 1979 na kunako mwaka 2006 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita akatembelea tena Uturuki.

Kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Novemba 2014, Baba Mtakatifu Francisko atafanya hija ya kichungaji inayopania kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kukata mzizi wa mambo ambayo bado yanakwamisha umoja kamili kati ya Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki.

Baba Mtakatifu anafanya hija hii ya kichungaji wakati kuna hali tete ya usalama huko Mashariki ya Kati, ambako bado vita, dhuluma na nyanyaso za kidini bado zinaendelea kusikika. Pamoja na hali hii tete, lakini bado kuna ushahidi wa uwepo wa Wakristo katika eneo hili, kumbe, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mambo mengine, itasaidia kuwatia moyo Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati, ili kuendelea kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya magumu wanayokabiliana nayo.

Padre Martin Kmetec, Mkapuchini ambaye kwa miaka mingi anaishi nchini Uturuki anasema, lengo kubwa la hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko ni kumtembelea ndugu yake katika Kristo Patriaki Bartolomeo wa kwanza, ili kuendelea kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene ulioanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Historia ya Makanisa nchini Uturuki bado inaonesha madonda makubwa na kwamba, kuna misigano ya kidini inayoendelea kujitokeza.

Kuna njama za kutaka kuligeuza Kanisa kuu la Mtakatifu Sofia kuwa tena Msikiti, hali ambayo inaweza kugumisha majadiliano na mahusiano ya kidini nchini Uturuki. Hivi karibuni, Patriaki Bartolomeo wa kwanza alitoa mhadhara kuhusu mchango wa Mtakatifu Yohane XXIII katika maisha na utume wa Kanisa, katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox.

Mtakatifu Yohane XXIII alionesha dira na mwelekeo wa Kanisa kwa siku za usoni na kwamba, Wakristo wanachangamotishwa kujikita katika hali ya unyenyekevu, ukweli na uwazi, huku wakimwachia Roho Mtakatifu kuwasaidia kufikia lengo la umoja kamili. Kanisa halina budi kusikitika kutokana na utengano ambao umedumu kwa kiasi kikubwa, lakini linapaswa kuwa na ujasiri wa kuangalia mbele kwa imani na matumaini, kama walivyofanya waasisi wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene, miaka hamsini iliyopita.

Kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014, Baba Mtakatifu Francisko alitembelea Yerusalemu, kama kielelezo cha kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana, kuzungumza na kusali na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu, hapo Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wakakutana pia na kusali pamoja, mwendelezo wa hija ya majadiliano ya kiekumene, huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anataka kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili wote waweze kuwa wamoja kadiri ya mapenzi ya Kristo mwenyewe. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kutembelea na kuzungumza na waamini wa dini ya Kiislam, changamoto endelevu ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kitamaduni kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, ili kweli amani, upendo, mshikamano na mafao ya wengi yaweze kupewa kipaumbele cha kwanza anasema Padre Martin Kmetec.







All the contents on this site are copyrighted ©.