2014-10-27 07:52:02

Wazazi msisahau dhamana na wajibu wenu kwa kisingizio kwamba mko "bize"


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Tunakukaribisha kwa mara nyingine tena katika kipindi hiki ambapo kwa uchache tutaangazia yaliyojiri wakati katika wa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. RealAudioMP3
Historia yatukumbusha kwamba, Mwenyeheri Papa Paulo VI, ndiye aliyeuendeleza Mtaguso huo na kuzisaini hati zote kumi na sita za mtaguso na zaidi sana, kwa roho ya ushujaa ulioongozwa na Hekima ya Kimungu, Papa huyu alisimamia mwanzo wa utekelezaji wa maamuzi ya Mtaguso.
Aliliongoza Kanisa Takatifu katika kipindi tete sana cha mpito, ambapo kutokana na maamuzi mbalimbali ya mababa wa Mtaguso mabadiliko makubwa yalipaswa kufanyika ili kuleta hewa mpya ndani ya Kanisa, kwa ajili ya usitawi wa Kanisa na kufanikisha utume wa Kanisa kwa nyakati zetu.
Kuongoza watu katika kipindi cha mpito si kazi rahisi. Kama wasemavyo waswahili: mazoea yana tabia ya kutokukubali mabadiliko mapema. Hakika, kutokana na hali ya kuzoea, sio wote waliweza kupokea mtaguso kwa utulivu. Katika kujipanga sawa, kulikuwa na mitikisiko na mipasuko midogomidogo ya ndani ya Kanisa.
Lakini Papa Paulo VI, alisimamia kidete kabisa utekelezaji wake naye mwenyewe akijibidisha haswa kubadili sura ya maisha na utume wa Papa. Alijidhihirisha kuwa ni Baba wa wote na Mchungaji wa Kondoo anayewatembelea kondoo hukohuko waliko. Ndiyo maana hakusita kufanya ziara ndefu za Kichungaji nje ya Italia.
Kwa nafasi hii ambapo sote tunaishangilia zawadi ya Mungu kwetu, kwa kuridhia mtumishi wake mwema na mwaminifu aandikwe katika kitabu cha wenye heri, tunapenda kutumia nafasi hii kukudokeza yaliyojiri wakati wa Mtaguso huo muhimu sana katika usitawi wa Kanisa.
Lengo letu: tunataka kuyapyaisha mafundisho ya mtaguso wa pili wa Vaticani, ili sote kwa pamoja tuendelee kusaidiana katika kutekeleza maagizo yake na zaidi sana kuuishi Mtaguso huo.
Mpendwa msikilizaji, tukumbuke kwamba, muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwake, , kunako tarehe 25 Januari 1959 akiwa katika Kanisa kuu la Mtume Paulo nje ya kuta za Roma, alitangaza adhima yake ya kuitisha wenye lengo la “kufungua” madirisha na kuleta hewa mpya ndani ya Kanisa kwa ajili usitawi wa Taifa zima la Mungu. Alipenda Kanisa lihuishwe katika wito na utume wake kwa watu wote.

Tofauti na Mitaguso iliyotangulia, mingi yake iliitishwa ili kujibu au kufafanua uzui fulani uliokuwa unajitokeza ndani ya Kanisa, na pia wakati mwingine kutatua matatizo fulani ya utengano. Lakini Mtaguso huu ambao ni wa kichungaji zaidi, ulikuwa ni wa kawaida kabisa, Kanisa likilenga kujitazama, kujirekebisha na kujiimarisha zaidi. Kanisa lilijipatia nafasi ya kujitathimini na kujiunda vizuri zaidi ili kutekeleza utume wake kama chombo cha wokovu wa mwanadamu.
Baada ya tangazo hilo zito na maandalizi yote kukamilika, Mtaguso huo ulifunguliwa rasmi tarehe 11 Oktoba 1962 na kufungwa tarehe 8 Desemba 1965, baada ya kuwa na vikao vizito vinne ambavyo vilikuwa vinaanza mwezi Oktoba na kuhitimishwa mwezi Desemba. Tukihesabu Mitaguso yote, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulikuwa ni wa 21.
Baada ya takriban miezi saba tu baada ya kuufungua Mtaguso huo Mkuu, Papa Yohane XXIII, aliitwa nyumbani kwa Baba tarehe ya 2 Juni 1963, akiwa ameongoza kikao kimoja tu, kile cha Ufunguzi. Tarehe 21 Juni 1963, Mwadhama Kardinali Giovani Baptista Montini, alichaguliwa kuwa Papa, akachukua jina la Paulo. Yeye aliamua kuuendeleza mtaguso ule na akasimamia vikao vitatu na kuufunga rasmi mwaka huo wa 1965.
Pamoja na lengo la kuyapyaisha mafundisho haya katika masikio yetu, tunapenda sauti hii ifike huko kwenye Kanisa la Nyumbani. Mtoto ni Malezi. Wazazi wa Paulo VI walikuwa ni watu wenye kazi na vyeo katika jamii kwa sababu ya hali yao ya usomi. Lakini pamoja na fanaka hizo, wazazi hawa hawakusahau wajibu wao wa kiutu, kiimani na kijamii. Hawakumsahau Mungu. Hivi nguvu ya malezi yao kwa watoto walipata kutokana na uhusiano wao na Mungu. Ni kwa sababu ya uzazi wao muwajibifu, watoto wakakua, wakasoma na kuifaa jamii na mmoja wao hata akaketishwa katika Kiti cha Mtume Petro.
Wazazi wapendwa, siku zetu hizi, kazi na utafutaji mali vinatunyang’anya upendo wetu kwa watoto. Nasi wenyewe kwa kisingizio cha kazi tunajivua wajibu wetu wa kuwalea vizuri watoto ili nao waje kuwa wazazi na wafanyakazi wazuri. Watu mashujaa wenye kumcha Mungu kama Paulo VI, hawashuki kutoka mbinguni, bali wanatoka katika familia zetu. Watoto wasipolelewa vizuri, vipaji vyao vitafichama na mwishoni wataonekana kama hawafai, kumbe ni sisi wazazi tumechangia kutokufaa kwako. Kumbuka, Malezi bora ndiyo msingi wa jamii iliyobora.
Kwa nafasi hii, tunapenda kuzidi kualikana kuzisoma hati za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili tuuishi mtaguso huo. Katika kipindi kijacho, tutakuletea kwa uchache yaliyomo katika hati hizo.
Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.