2014-10-25 07:35:55

SIGNIS yatambuliwa na Kanisa kuwa ni Chama cha Kitume Kimataifa!


Baraza la Kipapa la Walei, tarehe 24 Oktoba 2014 limetoa tamko ambalo linatambua Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki Duniani, kwa kifupi SIGNIS kuwa ni mojawapo ya vyama vya kitume kwa ajili ya Kanisa zima, katika ibada ya Neno la Mungu iliyoongozwa na Kardinali Stanislaw Rylko Rais wa Baraza la Kipapa la Walei na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa kutoka ndani na nje ya Vatican. SIGNIS iliundwa kunako mwaka 2001 baada ya kuunganisha Mashirika ya OCIC, lililoanzishwa mwaka 1928 na UNDA mwaka 1945 kushughulikia masuala ya mawasiliano.

Kardinali Stanislaw Rylko anasema, Kanisa linatambua mchango mkubwa uliokwisha kufanywa na SIGNIS katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu mawasiliano ya jamii, ndiyo maana Shirikisho hili limepewa hadhi na utambulisho wa Kanisa Katoliki, kwa kutambua dhamana na wajibu wake mbele ya umma.

Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, SIGNIS inashiriki katika mchakato wa kutetea, kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu; kwa kujielekeza zaidi katika masuala ya haki, amani nba upatanisho, kama sehemu ya utume wake ulimwenguni ili kuhakikisha kwamba, SIGNIS inashiriki kikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya mwanga wa Injili.

Kardinali Rylko anasema kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi, baadhi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii vimekuwa na mwelekeo hasi dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Kutokana na changamoto hii, Kanisa lina wajibu wa kuhakikisha kwamba, watu wanapata habari muhimu na za kweli kuhusiana na masuala mbali mbali yanayowazunguka, kwa kuzingatia haki na upendo, kwani ulimwengu umeumbwa kutokana na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kukombolewa na Yesu Kristo, aliyejisadaka kwa ajili ya mwanadamu, ili kumrudishia tena mwanadamu hadhi yake iliyokuwa imepotea kutokana na dhambi.

SIGNIS inachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inashiriki kikamilifu katika majiundo makini ya wanahabari, ili kweli waweze kuwa ni wanga wa mataifa na chumvi ya dunia kwa maneno na matendo yao yanayoonesha imani tendaji kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wanahabari kwamba, kazi yao inahitaji maandalizi makini, uzoefu na mang'amuzi ya ndani kwa kutafuta daima kile kilicho: kweli, chema na kizuri katika maisha ya mwanadamu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo mwamini anapata neema ya utakaso, changamoto ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha, dhamana inayopaswa kuendelezwa na SIGNIS katika maisha na utume wake ulimwenguni, kwa kuwajengea uwezo wanahabari ili kweli waweze kuwa ni watakatifu wanapotekeleza nyajibu zao za kila siku.

Wanahabari watafute daima mafao ya wengi wanapomhudumia mwanadamu na kwamba, SIGNIS inalo jukumu la kuwatangazia pia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, SIGNIS inawajibika kuwafunda wanahabari, kuwaunga mkono katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kusambaza habari kadiri ya mwanga wa Injili, ili kweli wanahabari waweze kuwa ni wahudumu makini wa binadamu katika mahitaji yake msingi.

Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii pamoja na viongozi wakuu wa Shirikisho la Wanahabari Wakatoliki, SIGNIS walitoa nasaha zao katika tukio hili muhimu sana kwa SIGNIS inapotambuliwa na Kanisa kama chama cha kitume kwa Kanisa zima, safari ndefu iliyoanza kunako mwaka 1928.







All the contents on this site are copyrighted ©.