2014-10-25 10:07:33

Miaka 50 ya Uhuru wa Zambia na changamoto zake!


Wananchi wa Zambia wanaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu walipojipatia uhuru wao kutoka kwa Mwingereza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyewawezesha kuendeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa kitaifa, amani, demokrasia, uzalendo, maendeleo na ustawi wa wengi.

Ni changamoto ya kuendelea kujikita katika mkakati wa kudumisha uhuru na upatanisho wa kitaifa ikikumbukwa kwamba, Zambia pia imepitia katika misukosuko mingi ya kisiasa katika kipindi cha miaka 50 tangu ilipojipatia uhuru wake.

Wananchi wa Zambia wanaendelea kuhamasishwa ili kuhakikisha kwamba, kweli utajiri na rasilimali za nchi zinatumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Zambia, si kama mwelekeo wa sasa unaotaka kuwanufaisha baadhi ya wananchi wa Zambia, huku wengi wao wakiendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini, magonjwa na njaa. Jubilee kiwe ni kipindi cha kuimarisha haki msingi za binadamu kwa kuwasaidia wananchi kumiliki ardhi, ili wajiharakishie maendeleo yao, sanjari na kudumisha utawala wa sheria na demokrasia ya kweli.

Hizi ni baadhi ya changamoto zilizotolewa na Padre Brian Chibuluma, mkuu wa taaluma kutoka Seminari kuu ya Mtakatifu Dominico, wakati wa Ibada ya pamoja kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa Zambia; Ibada ambayo imehudhuriwa pia na Makamu wa Rais wa Zambia Bwana Guy Scott, kwani kwa sasa Rais Michael Sata wa Zambia yuko nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Maadhimisho ya Jubilee ni fursa ya kujikita katika ujenzi wa nchi kwa kusoma alama za nyakati ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wananchi wengi wa Zambia ambao kwa sasa wana kiu na hamu ya maendeleo makubwa. Kanisa Katoliki linaipongeza Serikali ya Zambia kwa kuwekeza zaidi katika maendeleo ya watu kwenye sekta mbali mbali za maisha, bila kusahau maisha ya kiroho, kwa kujikita katika maadili na utu wema; toba, wongofu wa ndani na upatanisho, ili kujenga na kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kwani wananchi wote wa Zambia wanaunda Familia moja ya Mungu.

Sherehe za maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa Zambia zimehudhuriwa pia Rais mstaafu Dr. Keneth Kaunda muasisi wa Taifa la Zambia ambaye ameshangiliwa sana alipoingia kwenye Uwanja wa mashujaa wa Zambia, Ijumaa tarehe 24 Oktoba 2014.







All the contents on this site are copyrighted ©.