Kanisa linapenda kuhamasisha mchakato wa mabadiliko ya kweli katika jamii yanayosimikwa
katika haki
Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi
Jamii pamoja viongozi wa vyama vinavyotetea utu na heshima ya binadamu kutoka sehemu
mbali mbali za dunia, kwa pamoja wameandaa mkutano unaojadili kwa kina haki msingi
za binadamu, hususan kwa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watu ambao utu na
heshima yao vinaendelea kuwekwa rehani. Mkutano huu unaanza kutimua vumbi mjini Roma
kuanzia siku ya Jumatatu, tarehe 27 hadi tarehe 29 Oktoba, 2014.
Kardinali
Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani anasema, kuna watu wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii, hawa ni wale wanaotambulikana kutoka katika dunia au maskini,
"akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi". Hawa ni matokeo ya utandawazi usioguswa na
mahangaiko ya watu, wengi wao wakiwa ni vijana ambao hawana tena fursa za ajira na
wazee wanaoonekana kuwa kama kero kubwa kwa jamii kiasi cha kuizuia jamii "kula kuku
kwa mrija".
Hizi ni baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa
utandawazi usioguswa na mateso wala mahangaiko ya watu, changamoto kwa Mama Kanisa
kusikiliza kwa makini kilio cha haki na kujibu kilio hiki kwa nguvu. Ni mwaliko wa
kuwakumbatia na kuwashirikisha wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Huu ni
wajibu wa Kanisa na Jamii husika, ili kila mtu aweze kujisikia kuwa ni mdau na mtu
muhimu sana katika ujenzi wa jamii, ustawi na maendeleo ya watu katika medani mbali
mbali za maisha.
Kardinali Turkson anasema, jambo la msingi ni kusikiliza kwa
makini, sio tu mahangaiko na mateso ya watu hawa, bali pia matarajio na matumaini
yao pamoja na mikakati ambayo watu hawa wanatamani ifanyiwe kazi, kwa kutambua kwamba,
wao ni wadau wa kwanza katika utekelezaji wa mikakati hii katika maisha yao na wala
si watazamaji katika mchakato huu wa maendeleo. Ni watu wanaohitaji mabadiliko ya
dhati katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kitamaduni, ili waweze kujiunga
na kuunda makundi au vikundi vya kutekeleza mikakati hii.
Mkutano huu pamoja
na mambo mengine anasema Kardinali Turkson unajadili mambo makuu matano yaani: changamoto
zinazoendelea kujitokeza katika masuala ya makazi ya watu, fursa za ajira, ardhi,
uhalifu na mazingira. Mama Kanisa kwa upande wake, anapenda kuzimilisha changamoto
hizi kama sehemu ya utume wake kwa Watu wa Mataifa, ili kuhamasisha mabadiliko ya
kweli katika jamii, ili kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki.
Watu nao
kwa upande wao wanataka kushirikiana na Kanisa ili kuyachachua malimwengu katika ngazi
mbali mbali kwa kuwashirikisha watu ile nguvu ya upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi
Mungu na huruma iliyodhihirishwa na Yesu Kristo Mkombozi wa dunia.
Baba Mtakatifu
Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kushikamana na kuwasaidia maskini ili waweze
kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha. Huu ni mchakato endelevu wa mawasiliano
yanayojikita katika majadiliano, ushirikiano na uratibu katika ngazi mbali mbali.
Huu ni mwaliko kwa watu kushiriki kikamilifu katika mustakabali wa maisha yao kwa
siku za usoni.