2014-10-25 09:09:06

Jiepusheni na imani za kishirikina, rushwa na ufisadi; ili kujenga Kanisa


Kardinali Thèodore Adrien Sarr, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal, hivi karibuni wakati wa kufungua Mwaka wa Shughuli za kichungaji Jimboni mwake, ameitaka Familia ya Mungu kuwajibika barabara katika ujenzi wa Kanisa la Kristo kwa kuachana na mila na desturi ambazo kimsingi zinasigana na mwanga wa Injili. Kardinali amewataka waamini kuachana kabisa na mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati; mambo ambayo kimsingi ni hatari kwa utu, heshima na maisha ya mwanadamu.

Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuendelea kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani unaopaswa kupata chimbuko lake katika maisha ya mtu binafsi na jumuiya ya waamini, ili kweli kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na mayofu waweze kudhihirisha imani katika matendo, changamoto muhimu katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya mwanga wa Injili.

Waamini wanatakiwa kuachana na imani za kishirikina, ambazo zimekuwa ni chanzo cha kero na majanga mengi ndani ya jamii, kwa watu kudhani kwamba, kwa kufuata ushauri kutoka kwa waganga wa jadi wataweza kupata utajiri, kupandishwa vyeo au mafanikio makubwa katika maisha; mambo ambayo kimsingi ni ndoto za mchana, lakini cha kushangaza ni kuona kwamba, hata watu wenye imani na akili zao timamu bado wanajipanga "foleni" kwa kushiriki imani za namna hii.

Kardinali Sarr amekemea kwa nguvu zote rushwa na ufisadi, mambo ambayo kwa sasa yamekuwa ni "janga la kitaifa", licha ya kampeni kubwa zinazoendelea kufanywa na wadau mbali mbali. Hapa watu wanapaswa kujielekeza katika utekelezaji wa kanuni maadili, utawala wa sheria, bidii, juhudi na maarifa kama sehemu ya mchakato wa kujitafutia na kujiletea maendeleo endelevu na kwamba, katika maisha hakuna njia ya mkato, bali watu wajibidishe kutafuta maendeleo kwa njia ya jasho lao.

Kardinali Sarr anakumbusha kwamba, Kanisa ni mahali ambapo waamini wanapaswa kujichotea huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu; hapa waamini wajisikie kutoka katika undani wao kwamba, wanaweza kupokelewa, kupenda na kupendwa; kusamehe na kusamehewa pamoja na kuimarishwa kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na ushuhuda makini, kuwa kweli ni vyombo vya Uinjilishaji kwa njia ya maisha adili, matakatifu na manyofu; maisha ambayo yanapata mwanga na chimbuko lake kutoka katika Injili ya Kristo.

Waamini wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa kwa kutambua kwamba, Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi katika maisha na utume wa Kanisa; ndiye nguzo muhimu ya umoja, upendo na mshikamano katika Kanisa. Waamini wamekumbushwa kwamba, Yesu alikuja ulimwenguni ili kuwaunganisha, mwaliko kwa waamini kuonesha upendo na mshikamano kwa kutaabikiana na kusaidiana katika maisha, kila mwamini akichangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Kwa namna ya pekee, Kardinali Thèodore Adrian Sarr amewataka waamini kuhakikisha kwamba, wanalihudumia Kanisa kwa kutumia karama na mapaji mbali mbali waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu katika hija ya maisha yao na kamwe wasiwe ni chanzo cha kero na kinzani ndani ya Kanisa kwa kujitafuta wenyewe sanjari na kulihujumu Kanisa kutokana na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka.







All the contents on this site are copyrighted ©.