Baba Mtakatifu Francisko kukutana na wadau wa huduma kwa watu wenye matatizo ya afya
ya akili
Baraza la Kipapa la Wafanyakazi katika sekta ya afya, kuanzia tarehe 20 hadi tarehe
22 Novemba 2014 litafanya mkutano wake wa ishirini na tisa wa kimataifa mjini Vatican,
utakaoongozwa na kauli mbiu "Watu wenye matatizo ya afya ya akili". Watu wenye matatizo
ya afya ya akili na wale wanaowahudumia ndio walengwa wakuu wa mkutano huu wa kimataifa,
ili kubainisha mbinu na mikakati itakayoimarisha na kukoleza matumaini kwa watu wenye
matatizo ya afya ya akili pamoja na ndugu na jamaa zao wanaowahudumia.
Askofu
mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la Wafanyakazi katika sekta ya afya
anabainisha kwamba, huu ni mkutano utakaowashirikisha mabingwa na watalaam wa afya
ya akili kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kukabiliana na changamoto hizi katika
sekta ya afya. NI mkutano utakaozingatia masuala ya kisayansi, tiba, familia, taasisi
za elimu na huduma pamoja na kuwa na mwelekeo wa jumla kwa Serikali na Jamii husika.
Wawezeshaji
wa mkutano huu watashirikisha pamoja na mambo mengine masuala ya kijamii na kidini
yanayolenga kupata ufumbuzi wa matatizo na changamoto zinazoendelea kuwakumba watu
wenye matatizo ya afya ya akili. Mkutano huu utafunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu
itakayoongozwa na Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Uchumi mjini
Vatican.
Wajumbe wa mkutano huu watapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na
Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kuwashirikisha wafanyakazi mbali mbali kutoka katika
sekta ya afya, taasisi na vyama vinavyowahudumia wagonjwa. Kwa mara ya kwanza, Baba
Mtakatifu Francisko ataweza kukutana ana kwa ana na hali halisi ya watu wanaoteseka
kutokana na kudorora kwa afya ya akili katika mwelekeo wa kimataifa.
Kwa kukutana
na kuzungumza na Baba Mtakatifu wadau mbali mbali wataweza kushirikisha na kujipatia
matumaini na imani kwamba, Kanisa bado lina wajali na wala katika mahangaiko yao,
hawako pweke, bali kuna kundi kubwa la wadau wanaopenda kuwashirikisha na kuwamegea
mshikamano wa upendo unaojikita katika kanuni maadili na utu wema.