2014-10-24 12:08:46

Waonjesheni wengine fadhila ya upendo inayojikita katika unyenyekevu, ufukara na furaha ya kweli!


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi, tarehe 25 Oktoba 2014 anatarajiwa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Assunta Marchetti kuwa Mwenyeheri, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa huko San Paolo, Brazil. Mwenyeheri Sr. Assunta Marchetti alizaliwa kunako mwaka 1871 huko Lucca, Kaskazini mwa Italia, akiwa ni mtoto wa tatu kati ya watoto kumi na moja katika familia ambayo ilibahatika pia kuwa na Padre aliyejulikana kwa jina la Padre Giuseppe Marchetti.

Sr. Assunta ni mwanamke wa shoka aliyejipambanua kwa huduma makini kwa watoto maskini waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi, maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa kuanzisha Kituo cha Watoto Yatima huko San Paolo, Brazil. Sr. Assunta alijishughulisha kwa kiasi kikubwa na huduma kwa maskini, yatima na wagonjwa, lakini baada ya kushikwa na ugonjwa, afya yake ilianza kudorora na hatimaye, akiwa na umri wa miaka 77 akifariki dunia, kunako tarehe 1 Julai 1948.

Sr. Assunta alionesha fadhila ya upendo, akaguswa na mahangaiko ya watoto maskini, kiasi hata cha kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza, akiwaonesha na kuwaonjesha watoto hao, upendo wa kimama. Alishuhudia imani yake katika matendo, daima akitegemea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Aliwafundisha watoto kusali na kumtegemea Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani anasema Kardinali Angelo Amato, kiasi kwamba, shughuli hizi za kimissionari zikaacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wake nchini Brazil Aliwaonjesha watoto ukarimu wa mapendo, daima akitambua na kuiona ile sura ya Kristo mteswa katika nyuso za watoto wadogo, akapendwa na kuheshimiwa sana na watu kutoka ndani na nje ya Jimbo la San Paulo, Brazil.

Mwenyeheri Sr. Assunta Marchetti ameliachia Kanisa urithi mkubwa wa kutambua kwamba, upendo wa kimama ni huduma inayojikita katika unyenyekevu, sadaka na uvumilivu. Huu ni mwaliko anasema Kardinali Angelo Amato kwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha fadhila ya upendo inayojikita katika unyenyekevu, ufukara na furaha ya kweli.







All the contents on this site are copyrighted ©.