2014-10-24 15:20:11

China kuwekeza kwa nguvu nchini Tanzania


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa maendeleo ya haraka ya Jamhuri ya Watu wa China ni hamasa kubwa na ya kutosha kwa nchi za Afrika kuwa nazo zinaweza kuendelea katika kipindi kifupi kama zitaongozwa na sera sahihi za mageuzi ya kiuchumi.

Rais Kikwete ameyasema hayo, Ijumaa, Oktoba 24, 2014, wakati alipokutana kwa mazungumzo rasmi na Mwenyekiti (Spika) wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China, National People’s Congress (NPC) Mheshimiwa Zhang Dejiang, ikiwa ni moja ya shughuli za Mheshimiwa Rais katika ziara yake rasmi ya China.

Katika mazungumzo hayo kwenye Jengo la Bunge la Great Hall of the People mjini Beijing, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Dejiang: “China inatuhamasisha sana kwamba na sisi tunaweza kupata mabadiliko na maendeleo ya haraka ya wananchi wetu ili mradi tu tuweze kuwa na sera sahihi ambazo zinalenga katika kuleta mageuzi ya msingi na ya kweli kweli ya kiuchumi”.

Rais Kikwete amesema kuwa kwake yeye ambaye amekuwa anatembelea China kila baada ya wastani wa miaka minne, mabadiliko ya China yanatia hamasa kweli kweli kuwa nchi za Afrika pia zinaweza kuleta mageuzi makubwa ya maisha ya watu wake.

“Nilikuja hapa kwa mara ya kwanza mwaka 1980, na tokea wakati huo nimetembelea nchi hii kila baada ya miaka minne kwa wastani na kila nikija nashuhudia mabadiliko makubwa yasiyopimika na wala kufikirika. China ilikuwa nchi masikini sana wakati nilipofika hapa kwa mara ya kwanza lakini katika miaka 30 tu imebadilika kutoka nchi masikini na kuwa nchi iliyoendelea na yenye uchumi unaoshikilia nafasi ya pili kwa ukubwa duniani,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Tunawapongeza sana kwa juhudi ambazo zimewafikisheni hapa. Mnatuhamasisha na sisi kuwa ipo siku moja na sisi katika Afrika tutafikia hatua hii ya maendeleo.”

Naye Mheshimiwa Dejiang amemkubusha Rais Kikwete mazungumzo kati yao wakati walipokutana kwa mara ya kwanza miaka saba iliyopita Ikulu, mjini Dar es Salaam. Wakati huo, Mheshimiwa Dejiang alikuwa Katibu wa Chama Tawala cha Kikomunisti cha China katika Jimbo la Guangzhou, jimbo ambalo linaongoza katika China kwa kufanya biashara na Tanzania. Kati ya biashara zote ambazo Tanzania na China zinafanya, asilimia 60 inatokea Jimbo la Guangzhou.

Mheshimiwa Dejiang pia amepongeza mahusiano mazuri kati ya Tanzania na China katika miaka 50 tokea nchi hizo mbili kuanzisha uhusiano wa kibalozi Aprili 26, mwaka 1964. Mwenyekiti huyo wa Bunge pia amesema kuwa ujenzi wa Reli ya TAZARA unaendelea kuthibitisha urafiki baina ya watu wa China, Tanzania na Zambia na kuongeza kwa Tanzania kwa kuimarisha TAZARA na kwa kutilia maanani utajiri na raslimali zilizopo, ikiwemo nafasi ya kijiografia, utulivu na amani na idadi kubwa ya watu, Tanzania ina sifa ya kuwa nchi tajiri katika miaka isiyokuwa mingi ijayo.








All the contents on this site are copyrighted ©.