Tafakari ya neno la Mungu Jumapili ya 30 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa
Mpendwa mwana wa Mungu, msikilizaji wa Radio Vatican kipindi tafakari Neno la Mungu,
karibu tutafakari pamoja masomo Dominika ya 30 ya mwaka A wa Kanisa. Leo Neno la Mungu
linatualika kutafsiri na kuona katika kila siku ya maisha yetu mpango wa Mungu unaotualika
kukuza upendo kwake yeye na kwa jirani. Kwa kifupi ni mwaliko wa upendo ulio wa dhati.
Katika Somo
la kwanza toka kitabu cha Kutoka tunapata wajibu wa kwanza wa kutenda katika mpango
uleule wa upendo nao ni kuwaheshimu na kuwatunza maskini yaani watoto yatima, wajane
na wageni. Hawa kwa hakika ni kundi ambalo lahitaji msaada wa daima kwa maana, yatima
hawana wazazi, wajane hawana wenzi wao wa ndoa na wageni hawako nyumbani walikozaliwa
au wanakoishi na hivi wako safarini, ni mahujaji.
Mwandishi anakazia jambo
hili kwa maana kulikuwepo na hila na fitina dhidi ya kundi hili lisilo na nguvu katika
jamii. Anawakumbusha wana wa Israeli kuwa hata wao walikuwa wageni huko Misri na hivi
wakumbuke mateso waliyoyapata na kwa namna hiyo wataweza kuwasaidia wanaoteseka katikati
yao. Mwandishi anaweka mbele yetu onyo kali kuwa ni chukizo kwa Mungu kuwatesa na
kuwanyonya maskini.
Mpendwa mwana wa Mungu, leo hii hali ni ngumu katika jamii
yetu, yaani mateso kwa wajane yameongezeka kupita kiasi, watoto yatima wamekuwa ni
vichokoo katika jamii na hata wengine kuwa chanzo cha mtaji wa biashara. Wageni wakati
fulani hatuwapi huduma ya kufaa. Hili ndugu zangu ni chukizo kwa Mungu. Vilio vyao
ni vilio vya damu kwa Mungu kama damu ya Abeli. Mpendwa unayenisikiliza, naomba uache
kabisa jambo hili ni kinyume na Injili ya upendo.
Mtume Paulo anapowaandikia
Watesalonike akiendeleza shukrani zake kwao kwa sababu ya imani yao thabiti kwa Mungu
kiasi kwamba imekuwa kielelezo cha mapendo ya Mungu kwa jumuiya zinazozunguka jumuiya
yao, ni msaada kwetu wa kutuwezesha kugundua kuwa Injili ni kurudisha shukrani kwa
Mungu na kushirikishana mapaji kati yetu na majirani na si kuleta manyanyaso kwa walio
maskini.
Mtume anawashukuru Watesalonike kwa imani yao iliyojaa moyo wa kimisionari,
ulio upanuzi wa himaya ya Mungu inayozidi kueleweka na kufunuliwa wazi zaidi kwa njia
ya utume wao. Katika wajibu huo wa imani, matendo ya upendo ndiyo msingi wa maisha
ya kikristu. Mtume Paulo anatupa mwanga pia wa kuelewa kuwa katika utume wetu wa upendo
kwa vyovyote vile kutakuwa na upinzani kama walioupata watu wa Tesalonike, kumbe,
yatupasa kutumaini daima.
Mpendwa mwanatafakari, katika somo la Injili fundisho
msingi ni lile la amri ya upendo, yaani wajibu wa kila mmoja wetu kumpenda Mungu kwa
moyo, akili na roho na kisha kuwekeza upendo huu katika kiumbe kilichoumbwa katika
sura na mfano wa Mungu, yaani mwanadamu. Katika jamii ya kiyahudi zilikuwepo amri
613 na kati ya hizi 365 zilikuwa zinazuia watu wasifanye mambo mbalimbali katika jamii
yao na 248 zilikuwa zinaelekeza kipi cha kufanya katika jumuiya.
Sheria hizi
zilionekana kuwa na uzito sawa, ingawaje kulikuwa na kutokukubaliana katika hili.
Baadhi ya walimu walisisitiza kuwa kumpenda Mungu na jirani ndiyo iliyokuwa ya kwanza.
Tokana na shida hii Mafarisayo wanamwuliza Bwana, ipi ni amri kuu?
Bwana akijua
nini maana ya swali lao ambalo msingi wake ni usawa wa amri 613 na majaribu kwake,
anawaambia iliyo kuu ni kumpenda Mungu na jirani. Ndiyo kusema amri hii ni ufupisho
wa mafundisho ya amri zote, ni ufupisho wa mafundisho ya Bwana. Na hivi Bwana anakazia
njia ya kumpenda Mungu ni kwa njia ya jirani. Anaweka machoni pao kiumbe kitukufu
yaani mwanadamu, kilicho sura na mfano wake kielelezo cha mapendo yake kwa ulimwengu
na hivi njia ya kumpenda yeye. Jirani kama tulivyosikia katika kitabu cha kutoka ni
yatima, mgeni na mjane na mwanadamu kwa ujumla kiumbe cha Mungu.
Mpendwa, ni
wajibu wetu sasa kutambua kuwa kila siku tutafakaripo amri za Mungu mwisho wa tafakari
yetu unapaswa kuwa ni kumpenda Mungu na Jirani. Pamoja na hilo moyo, roho na akili
vinapaswa kujionesha katika imani na tumaini katika Mungu mmoja. Kumbe imani thabiti
inakusanya akili, moyo na roho zetu na kuziweka machoni pa Bwana mwabudiwa daima,
na yeye hutoa mwanga ambao huzaa upendo na sadaka kwa jirani. Tumsifu Yesu Kristo
na Maria.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.