2014-10-23 08:08:19

Askofu mteule Josefu Mlola kusimikwa rasmi tarehe 26 Oktoba 2014: Tunakuja Kigoma kuwashika mkono!


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anawaalika waamini na wananchi wa Kigoma katika ujumla wao kujiandaa kikamilifu pamoja na kuendelea kusali, ili tukio la kumweka wakfu Askofu mteule Josefu Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma liende kadiri ya mpango wa Mungu. RealAudioMP3

Anasema Maaskofu wanajiandaa kwenda Kigoma ili kumwekea mikono na kumkabidhi Jimbo. Ni siku ya shukrani kwa Baba Mtakatifu aliyewapatia waamini wa Kigoma mchungaji mkuu, kwa kutambua kwamba, hadi sasa bado kuna baadhi ya Majimbo Katoliki Tanzania yako wazi na hayajapata wachungaji wakuu.

Askofu mteule Josefu Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma anatarajiwa kuwekwa wakfu na hatimaye kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma hapo tarehe 26 Oktoba 2014 Jimboni Kigoma. Taarifa kutoka Jimboni humo inaoesha kwamba, Jumamosi asubuhi tarehe 25 Oktoba, msafara wa Askofu mteule Mlola utaanza safari kutoka Seminari kuu ya Kipalapala, Tabora ambako hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Gombera, utume aliouanza mwaka 2011 baada ya kuhamishwa kutoka Seminari kuu ya Segerea ambako alikuwa ni Gombera Msaidizi.

Askofu mteule na msafara wake, watapokelewa kwa shangwe na nderemo na waamini wa Jimbo Katoliki la Kigoma kwenye Kigango cha Usinge, Parokia ya Nguruka ambayo iko mpakani na Jimbo kuu la Tabora na baadaye watapata chakula cha mchana na kuendelea na safari yao kuelekea Kigoma.

Askofu mteule atasimama kuwasalimia waamini watakaokuwa kwenye Chuo cha Newman, ambayo kwa sasa ni Sekondari na kama mipango itakamilika, basi kinatarajiwa kuwa ni Chuo cha Ualimu. Hiki ni kituo kinachoendeshwa na Watawa wa Upendo.

Saa 10: 00 Jioni, Askofu mteule Josefu Mlola atatinga Jimbo Katoliki Kigoma. Saa 12: 00 Jioni atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Kigoma na baadaye yatafuata masifu ya jioni, ambamo Askofu mteule ataungama Kanuni ya imani pamoja na kula viapo vya utii wakati atakapokuwa anatekeleza dhamana yake ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, Jimbo Katoliki la Kigoma na pote pale atakapotumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kadiri ya mahitaji ya Kanisa. Masifu yanatarajiwa kuongozwa na Askofu Ludovick Josefu Minde wa Jimbo Katoliki Kahama.

Askofu mteule Josefu Mlola anatarajiwa kuwekwa wakfu katika Ibada ya Misa takatifu, Jumapili tarehe 26 Oktoba 2014, tukio ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya Maaskofu Katoliki Tanzania, viongozi wa Serikali kitaifa na kimkoa pamoja na wageni kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Kigoma. Ibada inatarajiwa kuongozwa na Askofu mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora.
Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Josefu Mlola alizaliwa tarehe 9 Januari 1966 huko Rombo, Mashati, Kilimanjaro. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa tarehe 12 Julai 1997. Jimbo Katoliki la Kigoma, limekuwa wazi tangu tarehe 27 Juni 2012, wakati huo, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipomteuwa Askofu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu na kumpatia dhamana ya kuwa Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.