2014-10-19 08:45:05

Wosia wa Papa Francisko kwa Viongozi wa Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru Mababa wa Sinodi pamoja na wale wote waliowezesha kufanikisha maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia. RealAudioMP3

Tukio hili limeonesha umoja na mshikamano katika hija ya pamoja, ambayo wakati mwingine iliwalazimu kuongeza mwendo ili kufikia malengo yaliyopangwa, lakini wakati mwingine, Mababa wa Sinodi walionekana kuchoshwa na safari hii, lakini wameweza kushinda kishawishi hiki kwa kujikita katika moyo na ari ya ushuhuda wa maisha ya kichungaji kwa kushiriki furaha na majonzi ya Familia ya Mungu wanayoiongoza.

Baba Mtakatifu ameyasema haya, Jumamosi jioni tarehe 18 Oktoba 2014 wakati alipokuwa anafunga rasmi vikao vya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia iliyoanza hapo tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014. Hija ya Mababa wa Sinodi imeonesha mshikamano katika kusaidiana, kuhudumiana na kufarijiana wakati wa kinzani na hali ya kukata tamaa kwa kuonesha moyo mgumu kiasi hata cha kushindwa kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi ya kufanya mabadiliko ya kweli katika maisha; hapa kumeonekana kinzani kati ya Mababa wanaojikita katika mapokeo na wasomi wanaotaka mabadiliko, mambo ya kawaida katika maisha na utume wa Kanisa; mambo ambayo yamekuwepo hata wakati wa Yesu.

Baba Mtakatifu anasema Kanisa lina dhamana ya kuganga na kuponya majeraha kutoka katika undani wake na wala si kuwapaka watu "mafuta kwa mgongo wa chupa". Hiki si kipindi cha kufanya miujiza kwa kugeuza mawe kuwa mikate, wala mikate kuwa mawe kwa kuwabeza wadhambi, wanyonge na maskini. Ni kishawishi cha mtu kutaka kushuka kutoka juu Msalabani, ili kuufurahisha umati wa watu wanaotaka kusikia maneno matamu, kiasi cha kutikisa amana na misingi ya imani kwa kutokuwa makini katika ukweli na uhalisia wa maisha ya watu.

Baba Mtakatifu anasema, yote haya ni mapitio ambayo Mababa wa Sinodi wameyaonja. Amesikiliza kwa umakini mkubwa hotuba zilizotolewa na Mababa wa Sinodi, hotuba ambazo zimejikita katika imani, ari na mwamko wa kichungaji; kwa kukazia Mafundisho Tanzu ya Kanisa; kwa kuonesha hekima na busara, ukweli na uwazi; mchango wa Kanisa katika maisha ya ndoa na familia mintarafu Sakramenti ya Ndoa inayojengeka katika misingi ya: umoja, udumifu, uaminifu na uhuru wa kupokea na kuitunza zawadi ya maisha.

Hapa Kanisa limeonesha ufundi wake kama Mama na Mwalimu kwa kudumisha misingi ya Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume, linaloundwa na watakatifu wa Mungu na wadhambi wanaopaswa kukimbilia na kuonja huruma ya Mungu, ili kuwaganga wanadamu kwa divai na mafuta safi. Hili ndilo Kanisa la Kristo linalojibidisha kuwa aminifu kwa Kristo mchumba wake na kwa Mafundisho Tanzu. Kanisa halioni kinyaa kushirikiana na wadhambi, ili liweze kuwasaidia kusimama na kuendelea na safari ya maisha yao ya kiroho, tayari kuingia katika Yerusalemu mpya.

Hii ni changamoto ya kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake kwa kujikita katika Injili, upendo, umoja na mshikamano wa kidugu chini ya usimamizi na maongozi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa kutambua kwamba, anayo dhamana ya kulihudumia Kanisa la Kristo. Ikumbukwe kwamba, Kristo ndiye anayeliongoza, lilinda na kulirekebisha Kanisa kwani analipenda upeo! Viongozi wa Kanisa wanashiriki dhamana hii wanayopaswa kuitekeleza kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, huku wakionesha upendo na uhuru kamili unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo mwenyewe.

Viongozi wa Kanisa waongoze watu wao kwa upendo kama alivyofanya Kristo mchungaji mwema, wakionesha furaha, ukweli na uwazi; wakiwa na jicho la pekee kwa maskini, wadhambi, wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili waweze kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Kanisa ni la Kristo, viongozi wake wanatumwa kulilinda na kulihudumia na wala hii si mali yao bali wamekabidhiwa na Kristo mwenyewe, mwaliko wa kuonesha utii kwa mapenzi ya Mungu, Injili na Mapokeo ya Kanisa kwa kuweka kando kabisa mafao na vionjo vya mtu binafsi.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hotuba yake iliyosheheni utajiri mkubwa wa hekima na busara ili kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Anasema, Mababa wa Sinodi wanao mwaka mzima mbele yao ili kuendelea kufanya tafakari ya kina ili kupata mwanga zaidi wa maisha ya kiroho, ili hatimaye, kupata suluhu ya kweli katika kukabiliana na matatizo na changamoto ambazo familia zinakumbana nazo; ni mwaliko wa kutoa majibu muafaka kwa mambo yanayokatisha tamaa na kuzima tunu bora za maisha ya ndoa na familia. Kuna mwaka mzima wa kutafakari kuhusu Hati ya Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, ambayo kwa sasa inawasilishwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu kama "Lineamenta", "Mwongozo" wa Kazi.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.