Wekezeni kwenye fursa za ajira miongoni mwa vijana Barani Afrika!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Serikali ya Tanzania imefungua milango
kwa wawekezaji kwenye sekta zote lakini mkazi unaelekezwa zaidi kwenye sekta ya afya,
kilimo hasa usindikaji mazao, nishati na miundombinu. Ametoa kauli hiyo Jumatatu,
Oktoba 20, 2014) wakati akishiriki Mjadala wa Marais (Presidential Keynote Panel)
kuhusu fursa za uwekezaji barani Afrika uliolenga kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo
barani Afrika hasa katika nchi za Tanzania, Uganda, Ghana na Rwanda ambao umeanza
Jumatatu kwenye hoteli ya Savoy, jijini London, Uingereza. Waziri Mkuu aliwasili
jijini London jana mchana kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi unaohusu uwekezaji barani
Afrika (The Global African Investment Summit – TGAIS) kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete
na ameshiriki mjadala huo pamoja na Rais John D. Mahama wa Ghana, Rais Yoweri Museveni
wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda. “Tunahitaji wawekezaji kwenye sekta nyingi
lakini zaidi kwenye sekta ya afya katika vyuo vya tiba na uuguzi ili tupate watumishi
wa kutosha, utengenezaji wa madawa na vifaa vya hospitali na ujenzi wa hospitali,”
alisema. Aliyataja maeneo mengine ya kipaumbele kuwa ni kilimo na na hasa usindikaji
wa mazao, hasa ikizingatiwa kwamba asilimia kubwa ya Watanzania inategemea kilimo
kwa kujikimu. “Watanzania wengi bado wanategemea kilimo kama njia yao kuu ya uzalishaji,
tunahitaji pia kupata umeme wa kuendesha viwanda kutokana na gesi, makaa ya mawe pamoja
na geo-thermal,” aliongeza. Akizungumzia kuhusu uwekezaji kwenye miundombinu, Waziri
Mkuu alieleza Serikali ilivyojipanga kujenga reli mpya yenye urefu zaidi ya km. 2,000
kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, reli ya kutoka Tanga kupitia Arusha hadi Mwanza
na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo pamoja na uimarishaji wa bandari za Tanga, Mtwara
na Dar es Salaam. Kwa upande wao, Marais wa Ghana, Uganda na Rwanda walielezea
fursa zilizopo nchini mwao kwenye maeneo ya madini, miundombinu ya barabara na reli,
umeme, na teknolojia ya habari na mawasiliano. Mapema, akiwakaribisha wajumbe wa
mkutano huo wa siku mbili, Mwenyekiti wa mkutano huo, Rais mstaafu wa Nigeria, Bw.
Olesegun Obasanjo alisema Bara la Afrika lina nafasi kubwa ya kuendeleza sekta za
maenedeleo kupitia uwekezaji maliasili, Kilimo na usindikaji mazao, nishati na utalii. “Nchi
zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara zina fursa nyingi za uwekezaji na siyo hizi nne
ambazo zimewakilishwa leo hapa za Tanzania, Uganda, Ghana na Rwanda. Kuna miradi yenye
thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 200 ambayo itapata fursa za kunadiwa
kwa wawekezaji kupitia mkutano huu,” alisema. “Nimewaalika Marais kutoka nchi hizi
nne ili watupe mwanga wa kile tunacheweza kufanya katika nchi zao... lakini vilevile
tutambue katika Bara la Afrika kuna vijana wengi ambao ni zaidi ya asilimia 60 ambao
hawana kazi. Tutakuwa tumepotoka tusipoliangalia kundi hili. Ni lazima miradi inayotafutiwa
wawekezaji ilenge kuleta ajira kwa vijana wetu, wapate kipato (wealth creation) na
technology transfer,” alisema. Mkutano huo unahudhuriwa na wakuu wa makampuni na
taasisi za kibiashara zaidi 400.