Ushirikiano wa kiteknolojia usaidie kudumisha amani na usalama!
Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa,
hivi karibuni akichangia mada kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Mataiafa kuhusu ushirikiano
wa kimataifa anabainisha kwamba, imani inaweza kuisaidia sayansi kutambua na kuthamini
kazi kubwa ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa kutunza na kuiendeleza kwa ajili
ya mafao ya wengi, lakini kwa kuwa na mtazamo wa pekee kwa ajili ya maskini, ili nao
waweze kufaidika na vitega uchumi vinavyofanywa sehemu mbali mbali za dunia.
Askofu
mkuu Bernadito Auza anasema, ushirikiano wa kimataifa unagusa haki miliki ya kiakili,
leseni na matumizi sahihi ya anga la kimataifa, linalohifadhi teknolojia kubwa ya
mawasiliano duniani, kikolezo muhimu sana katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya
kijamii, lakini hadi sasa eneo hili limekuwa ni chanzo cha kinzani za kiuchumi na
kijamii badala ya kujikita katika mafao ya wengi pamoja na amani duniani. Kanuni maadili
ya Jumuiya ya Kimataifa katika matumizi anga la kimataifa ni muhimu sana katika mchakato
unaopania kukuza na kudumisha amani kwa kudhibiti biashara haramu ya silaha, inayotishia
amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa.
Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano
huu, unaipongeza Jumuiya ya Kimataifa kwa kucharuka katika mikakati ya kuifahamu sayari
dunia na mazingira yake na kwamba, ufahamu na maarifa haya yawajengee watu uwezo wa
kulinda na kutunza mazingira kwa kubadili mfumo wa maisha, ili dunia iweze kuwa ni
mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Teknolojia isaidie kupambana na ujinga, maradhi
na umaskini na kamwe teknolojia hii isiwakandamize watu kwa kulazimisha kufuata tamaduni
na tunu msingi za maisha kutoka kwa Jamii nyingine, kwa kisingizio cha kuwa na nguvu
ya kiteknojia. Anga linapaswa kutambulika kuwa ni sehemu ya urithi wa Jumuiya ya Kimataifa.
Watu wazingatie kanuni maadili, ili urithi huu uweze kuwafaidisha watu wengine kwa
siku za usoni.