Baada ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia yaliyoanza
hapo tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014, yakiongozwa na kauli mbiu "Changamoto za
kichungaji kuhusu familia mintarafu Uinjilishaji, Mababa wa Sinodi wametoa ujumbe
kwa Familia ya Mungu sehemu mbali mbali duniani wakionesha umoja na mshikamano wao
wa dhati na Baba Mtakatifu Francisko wakati wote wa maadhimisho ya Sinodi, kwa kutambua
kwamba, Yesu Kristo ni njia, ukweli na uzima. Mababa wa Sinodi wanazishukuru familia
zote zinazoendelea kuonesha uaminifu, imani, matumaini na mapendo.
Mababa wa
Sinodi wanasema hata wao, wamezaliwa na kukulia katika familia, huku wakiwa na historia
na makando kando mbali mbali. Kama viongozi wa Kanisa wamekutana na kuishi na na familia
ambazo zimesimulia na kuonesha kwa njia ya ushuhuda wa matendo uzuri na matatizo ya
familia. Maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu yalianza kwa kutuma
maswali dodoso kwa watu sehemu mbali mbali za dunia, ili kusikiliza kwa makini uzoefu
na mang'amuzi mbali mbali ya kifamilia.
Majadiliano kati ya Mababa wa Sinodi,
yamekuwa ni utajiri mkubwa kati yao katika mchakato wa kutambua ukweli kuhusu maisha
ya kifamilia. Mababa wa Sinodi wanaziambia Familia kwamba, Yesu anasimama mlangoni
pao huku akibisha hodi, ikiwa kama watasikiliza sauti yake, atakuja na kula pamoja
nao. Yesu hadi leo hii anaendelea kupiga hodi katika barabara na mitaa ya miji na
majiji mbali mbali kama alivyofanya alipokuwa akiishi katika Nchi Takatifu.
Mababa
wa Sinodi wanakiri kwamba, katika nyumba za waamini kuna mwanga na giza; kuna changamoto
kubwa, wakati mwingine za kukatisha tamaa. Giza hili limekuwa nene kiasi kwamba, linawatendea
vibaya na kusababisha wanafamilia kutenda dhambi. Changamoto kubwa ni uaminifu miongoni
mwa wanandoa. Hii inatokana na kumong'onyoka kwa imani na tunu msingi za kimaadili;
ubinafsi, mahusiano tenge, msongo wa mawazo na ukosefu wa tafakari ya kina; haya ni
mambo yanayozikumba familia. Kuna baadhi ya wanandoa wamekosa uvumilivu, hawana uhakika
wa mambo; hawana tena moyo wa kusamehe, upatanisho na sadaka. Huu ndio mwanzo wa kuporomoka
kwa ndoa na hivyo kusababisha kuibuka kwa mahusiano mapya, wanandoa wapya pamoja na
ndoa mpya, kiasi cha kugumisha maisha ya kifamilia mintarafu Ukristo.
Mababa
wa Sinodi wanakiri kwamba, kuna hali ngumu kwa wanandoa kuishi kwa pamoja kutokana
na magonjwa yanayowaandama watoto, magonjwa makubwa, uzee au kifo cha wapendwa ndani
ya familia. Pamoja na changamoto zote hizi, bado hata hivyo kuna familia ambazo zimedumu
katika uaminifu na kuendelea kuishi katika majaribu haya kwa ujasiri, imani na mapendo,
kwa kutambua kwamba, hivi si vikwazo vinavyoweza kusababisha kinzani, bali ni zawadi
inayowasaidia kumwona Yesu Kristo mteseka katika hali kama zile.
Mababa wa
Sinodi wanasema kwamba, kuna familia ambazo zinakumbana na athari za mtikisiko wa
uchumi kimataifa, hali ambayo inadhalilisha utu na heshima ya binadamu; ukosefu wa
fursa za ajira jambo linalowanyima uwezo wa kuhudumia familia zao hata kwa mambo msingi;
kundi kubwa la vijana wasiokuwa na kazi, vijana ambao wanaweza kutumbukia kwa urahisi
katika matumizi haramu ya dawa za kulevya na makosa ya jinai.
Mababa wa Sinodi
wanaona mbele yao familia maskini za watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao ili kutafuta
hali nzuri zaidi ya kuishi; familia zinazoteseka na kudhulumiwa kutokana na imani
yao, tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; familia ambazo zimeathirika kutokana
na vita na kinzani za kijamii. Kuna wanawake wanaodhulumiwa na kunyanyaswa utu na
heshima yao kutokana na: vipigo, biashara haramu ya binadamu bila kusahau nyanyaso
za kijinsia zinazofanywa na watu ambao wamekabidhiwa dhamana ya malezi na makuzi;
wanazikumbuka familia zote zinazonyanyasika na ambazo zinakabiliwa na matatizo makubwa.
Mambo
yote yanayonesha ile hamu ya kutaka kuwa na utamaduni wa maisha bora, lakini watu
hawaguswi na mahangaiko haya. Mababa wa Sinodi wakiwa wameguswa na mahangaiko ya familia
zote hizi, wanazitaka Serikali husika na Mashirika ya Kimataifa kusimama kidete kulinda
na kutetea haki za familia kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.
Yesu alitamani
kuliona Kanisa lake likiwa na malango wazi kwa ajili ya kuwapokea wote wanaotaka kuingia
humo bila ya kumtenga au kumbagua mtu awaye yote. Mababa wa Sinodi wanawashukuru kwa
namna ya pekee, wachungaji, waamini na Jumuiya ambazo ziko tayari kuwasindikiza pamoja
na kujitwika mzigo wa matatizo ya ndani na yale ya kijamii yanayowakabili wanandoa
na familia zao.
Pamoja na mambo yote haya bado kuna mwanga wa matumaini wanasema
Mababa wa Sinodi, mwanga unaoendelea kung'ara katika medani mbali mbali za maisha,
ili kuupatia moyo joto; ni mwanga unaojionesha kwa wachumba wanapoamua kufunga ndoa
ili kushirikishana upendo kati ya bwana na bibi kama unavyosimuliwa kwenye Maandiko
Matakatifu, hawa ni watu wanaokamilishana na kusaidiana licha ya tofauti zao msingi.
Hapa
ni mwanzo wa safari ya uchumba, kipindi cha kusubiri na kujiandaa kwa makini na kukamilishwa
katika maagano ya ndoa yanayotiwa muhuri kwa uwepo na neema ya Mungu. Ni safari inayotambua
tendo la ndoa, wema na uzuri unaovuka hata umri wa ujana kwa kutambua kwamba, upendo
kwa asili ni jambo linalodumu kiasi hata cha kujisadaka maisha kwa yule anayependwa.
Kwa mwanga huu, upendo wa maisha ya ndoa ni wa pekee na usiofutika; unaendelea kudumu
licha ya matatizo na mapungufu ya kibinadamu; huu ni muujiza wa pekee na unaogusa
watu wengi.
Mababa wa Sinodi wanasema kwamba, upendo huu unadumishwa kwa njia
ya mwendelezo wa kizazi kwa kutoa maisha mapya ya Kimungu katika Sakramenti ya Ubatizo;
elimu na malezi ya watoto. Ni upendo wenye nguvu ya kutoa maisha, hisia, tunu msingi
na mang'amuzi mapana hata kwa wale ambao hawakubahatika kupata watoto. Familia zinazoishi
katika ushuhuda wa mwanga huu ni ushuhuda tosha kabisa kwa wengi na hasa zaidi miongoni
mwa vijana.
Katika safari hii ya maisha kuna wakati ambapo wanandoa wanajisikia
kuchoka na hata wakati mwingine kuanguka chini, lakini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu
bado anawasindikiza, hali inayojionesha katika majadiliano kati ya wanandoa; kati
ya wazazi na watoto wao; kati ya ndugu na jamaa. Uwepo wa Mungu unajidhihirisha kwa
kuishi na kutafakari kwa pamoja Neno la Mungu; Sala za familia, pamoja na kufurahia
maisha pale nafasi inapopatikana katika siku.
Hapa kuna dhamana endelevu ya
kufundana katika imani, maisha mema ya Kiinjili na utakatifu. Utume huu wakati mwingine
wanashiriki mabibi na mababu, kiasi cha kuonesha Familia kama Kanisa dogo la nyumbani,
inayoendelea na kupanuka kwa kushirikiana na familia nyingine zinazounda Jumuiya ya
Kikanisa. Wanandoa Wakristo wanaalikwa kuwa kweli ni walimu wa imani na mapendo kwa
wanandoa vijana.
Mababa wa Sinodi wanasema kwamba, kuna umoja na mshikamano
wa kidugu unaojikita katika upendo, sadaka na ujirani mwema, kwa kuwajali maskini;
wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; wapweke, wagonjwa, wageni na familia ambazo
zinajikuta zikikabiliana na kinzani pamoja na migogoro mbali mbali, kwa kusukumwa
na Neno la Mungu kwamba, kuna faraja kubwa kutoa kuliko kupokea. Hii ni zawadi kubwa,
ni ujirani, ni upendo na huruma na kwamba, ni ushuhuda wa ukweli, mwanga na maana
ya maisha.
Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu linaloadhimishwa kila
Jumapili ni kusanyiko linalowaunganisha watoto wote na Mungu pamoja na jirani zao
ndani ya Kanisa kama Familia ili kwa pamoja kuweza kushiriki meza ya Bwana. Yeye anajisadaka
kwa ajili ya wote, mahujaji wanaotembea katika historia ili hatimaye kuweza kukutana
na Yesu Kristo atakapokuwa yote katika yote.
Mababa wa Sinodi katika awamu
hii ya kwanza wamejadili pamoja na mambo mengine jinsi ya kuzisindikiza familia katika
shughuli za kichungaji na maisha ya Kisakramenti kwa wana ndoa walioachana na kuoa
au kuolewa tena. Waamini wanaombwa na Mababa wa Sinodi kuendelea kuwasindikiza katika
maadhimisho ya Sinodi ya kawaida ya Maaskofu itakayoadhimishwa mwaka 2015.
Mababa
wa Sinodi wanaziombea familia zote ulinzi wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu
nao wanapenda kusali kwa ajili ya kuwaombea nguvu na hekima ili kweli familia ziweze
kuwa na uhuru na umoja; wazazi waweze kupata nyumba ambamo kuna amani na watoto wakiwa
kweli ni kielelezo cha imani na matumaini na kwamba, vijana waoneshe ujasiri, uwajibikaji
na uaminifu.
Mababa wa Sinodi wanawaombea watu wote ili waweze kupata riziki
kwa jasho lao wenyewe; waonje utulivu wa maisha ya kiroho, huku wakiwa na mwanga angavu
wakati wa giza la maisha. Mwishoni, Mababa wa Sinodi wanawaombea watu wote kuona Kanisa
linalostawi daima likiwa aiminifu na lenye kuaminika; mji wenye haki na utu; dunia
inayopenda ukweli, haki na huruma.
Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.