2014-10-20 15:06:54

Rais Kikwete atupa "madongo" kwa waandishi wa habari wanaoendekeza "kikandamizio cha habari"


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewataka waandishi wa Bara la Afrika kutokujihusisha na rushwa, ili wawe na nguvu za kutosha za kiroho kuwanyoshea vidole watu wengine. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa wingi mkubwa wa vyombo vya habari nchini unathibitisha kuwa Serikali yake inaendelea kulea na kukuza uhuru wa vyombo vya habari ambavyo vina uhuru wa kusema lolote bila kuingiliwa na serikali.

Rais pia amesema ukweli kuwa Serikali yake haikagui ama kusoma magazeti kabla ya hajachapishwa, ili kufuta habari zenye walakini (censorship) ni ishara nyingine tosha ya kukua na kuimarika kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini. Rais Kikwete ameyasema hayo, Jumamosi, Oktoba 18, 2014, wakati alipozungumza kwenye hafla kubwa na ya kuvutia ya Utoaji wa Tuzo la Mwandishi Bora wa Habari wa Afrika (CNN-Multichoice African Journalist Awards) kwa mwaka huu wa 2014 iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City Convention Centre mjini Dar Es Salaam.

Rais Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi katika halfa hiyo ambayo huandaliwa kila mwaka na Shirika la Habari la Kimataifa la CNN pamoja Kampuni ya Multichoice aliwaambia wageni kwenye hafla hiyo: “Kaka zangu na dada zangu katika vyombo vya habari, endeleeni kufanya kazi nzuri. Ushauri wangu wa unyenyekevu kabisa kwenu, ni kuwataka muwe waandishi wenye kuwajibika, wenye kuongozwa na maadili, wenye weledi na wenye uadilifu. Tumieni nguvu ya vyombo vya habari kwa haki na kwa nia ya kulinda na kuendeleza umoja na utulivu,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Epukeni kutukuza ghasia na kuchochea misuguano na migongano katika jamii. Zaidi ya yote hakikisheni kuwa mnakuwa wasafi wasiokula rushwa, ili muweze kuwa na ngvu za kiroho kuwanyoshea vidole wengine.” Kuhusu uhuru wa habari nchini Tanzania, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania inalichukua jambo hilo kwa uzito mkubwa. “Mimi binafsi, nimefanya mengi katika kukuza na kulea uhuru wa habari nchini. Ninafurahi kuona kuwa uhuru wa habari na vyombo vya habari unazidi kukua na kuimarika kila siku ipitayo. Leo, tuna vyombo vya habari vingi – vituo 29 vya televisheni, vituo 94 vya redio na magazeti 825 kulinganishwa na televisheni moja, redio tatu na magazeti matatu tu mwaka 1992.”

Ameongeza Rais kikwete: “Na lazima kukumbuka kuwa katika idadi hiyo yote, Serikali inamiliki kituo kimoja tu cha televisheni, magazeti mawili na redio moja tu. Wingi wa magazeti nchini, una maana ili mtu aweze kununua magazeti yote ya kila siku ni lazima atumie dola za Marekani kati ya 20 na 30 kila siku.”

Mshindi wa Tuzo hilo mwaka huu amekuwa ni Mpiga Picha wa Kujitegemea Joseph Mathenge kutoka Kenya ambaye picha zake za magaidi kuvamia na kuteka Duka kubwa la Westgate la Nairobi, Kenya ziliiwezesha dunia kuona na kujua unyama wa magaidi hao. Bwana Mathenge pia amekuwa mshindi wa Tuzo la Mohamed Amin la Upigaji Picha. Aidha walikuwepo washindi wengine kwa tuzo za Mazingira, Habari za Jumla za Lugha ya Kifaransa, Biashara na uchumi ya Coca Cola, Tuzo la Afya na Tiba la MSD ya Afrika Kusini, Uhuru wa Habari, Mohamed Amin la Picha, Nishati na Miundombinu, Tuzo la Habari za Jumla za Lugha ya Kireno, Tuzo la Habari Bora na Tuzo la Uandishi wa Habari za Michezo.

Mtanzania pekee kuingia fainali miongoni mwa washindani 23 walioingia fainali alikuwa ni Dickson Ng’hily wa gazeti la The Guardian. Akimtakia heri kabla ya kutangazwa washindi, Rais Kikwete alisema: “ Ninayo furaha kutambua kuwa mmoja wetu Bwana Dickson Ng’hilly kutoka Gazeti la The Guardian ni miongoni mwa waliofikia hatua ya mwisho kuwania Tuzo. Namwomba Mungu kuwa siku imalizike vizuri kwake, na ikitokea kuwa hakuwa mshindi bado litaendelea kuwa jambo la heshima na fahari kwetu kuwa ameweza kufikia hatua hii.”


Wakati huo huoRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jumamosi, Oktoba 18, 2014, ametoa kamisheni kwa maofisa wanafunzi 23 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao wamehitimu mafunzo yao ya uofisa katika kozi ya 54/13-DRC kwenye Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA) Monduli, Mkoani Arusha.

Sherehe hiyo iliyofanyika chuoni hapo imehudhuriwa pia na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mheshimiwa Joseph Kabila Kabange ambaye ameshuhudia maofisa 437 wa Jeshi la DRC wakihitimu mafunzo kwenye Chuo hicho. Hiyo ni mara ya kwanza kwa maofisa wa Jeshi la DRC kupata mafunzo TMA lakini Tanzania na DRC zimekuwa na mahusiano katika eneo la mafunzo ya kijeshi na mwaka 1997-1998, maofisa wa JWTZ walifundisha askari wa Jeshi la Congo.

Akizungumza kwa ufupi katika sherehe hizo, Rais Kabila amemshukuru Rais Kikwete na Watanzania kwa kuisaidia DRC kuwafundishia wanajeshi wake na hivyo kuiongezea nchi hiyo uwezo wa nchi hiyo kulinda mipaka na amani yake.

“Maofisa hao mliwafundisha hapa Tanzania watachangia sana kuimarisha ulinzi wa Congo na uwezo wake kukabiliana na adui zake ambao ni wengi. Mchango wa Tanzania utawasaidia wananchi wa Congo kuimarisha ulinzi na usalama wao ili wapate muda zaidi wa kushughulika na maendeleo. Mheshimiwa Rais na Watanzania wote nawashukuruni kwa mchango wenu huu,” amesema Rais Kabila.








All the contents on this site are copyrighted ©.