2014-10-19 14:48:23

Mwenyeheri Paulo VI


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 19 Oktoba 2014 katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuhitimisha maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia; Kumtangaza Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI kuwa Mwenyeheri pamoja na maadhimisho ya Siku ya themanini na nane ya Kimissionari Duniani. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa waamini kutoka ndani na nje ya Italia.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amewaambia waamini kwamba, Yesu aliweza kuwajibu ipasavyo Mafarisayo waliokuwa wanamuuliza maswali huku wakitaka kumjaribu kuhusu misimamo yao ya maisha, utajiri, nafasi na upendeleo wao wa kijamii, madaraka na umaarufu wao. Haya ni mambo ambayo ni endelevu kwa watu wa nyakati mbali mbali.

Yesu anawakumbusha waamini kwamba, Mungu ni Mungu, kumbe, wanapaswa kumfahamu na kumkiri mbele ya mamlaka yoyote ile, kwani Yeye ni Bwana na wala hakuna mwingine zaidi yake. Huu ndio upya na ukweli ambao waamini wanapaswa kuugundua kila siku ya maisha yao, kwa kushinda kishawishi cha woga ambacho waamini wakati mwingine wanakumbana nacho Mungu anapowashangaza katika maisha yao.

Mwenyezi Mungu anaendelea daima kumshangaza mwanadamu kwa kumwonesha na kumwongoza katika njia ambazo kamwe hakuweza kufikiria hata kidogo, kwani daima anapenda kuwapyaisha ili kweli Wakristo waweze kuishi upya wa Mungu na Injili ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake na kwamba, kwa hakika, Mungu anapenda upya. Hii ina maana ya kujifungua mbele ya mapenzi yake na kujisadaka bila ya kujibakiza ili kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika huruma, upendo na amani.

Baba Mtakatifu anasema hiki ndicho kiini cha nguvu inayowawezesha waamini kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa; hapa ni chemchemi ya matumaini kwani matumaini ya Mungu kamwe hayawezi kuukimbia ukweli na wala hayana ukinzani, bali yanampatia Mungu kile kilicho cha Mungu. Ndiyo maana Mkristo anaishi ukamilifu wa maisha yake kwa kuonesha ujasiri katika kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu anasema, Sinodi maana yake ni kutembea kwa pamoja. Viongozi wa Kanisa na Waamini walei kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamepaaza sauti zao mjini Vatican katika mchakato wa kutaka kuzisaidia familia nyakati hizi kutembea katika misingi ya Injili, huku zikimwangalia Yesu. Hiki ni kielelezo cha Sinodi na mshikamano wa kichungaji, jambo ambalo limewawezesha kuonja nguvu ya Roho Mtakatifu anayeliongoza na kulipyaisha Kanisa, ili liweze kuganga madonda yanayovuja damu na kuwapatia matumaini wale wote waliovunjika moyo.

Baba Mtakatifu anasema, ndiyo maana Mama Kanisa kwa njia ya maneno ya Mtakatifu Paolo anapenda kuwashukuru wote na kuwakumbuka kwa njia ya sala. Roho Mtakatifu amewawezesha Mababa wa Sinodi kutekeleza dhamana na wajibu wao katika uhuru na unyenyekevu unaojikita katika kipaji cha ugunduzi pamoja na kuliendeleza Kanisa katika maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya kawaida ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2015.

Mababa wa Sinodi wamepandikiza na wataendelea kupandikiza mbegu ya matumaini kwa unyenyekevu na uvumilivu mkuu ukweli kwamba, Yesu mwenyewe ataweza kukuza mbegu iliyoapndwa katika miyo ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema katika tukio la kumtangaza Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI kuwa Mwenyeheri, anakumbuka fika maneno aliyosema wakati wa kuunda rasmi maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, ili kusoma alama za nyakati na hatimaye kupata njia na mbinu za kupambana na changamoto mbali mbali kutoka katika Jamii. Leo Kanisa linapenda kumshukuru kwa dhati Papa Paulo VI kwa unyenyekevu na ushuhuda wake wa kinabii unaonesha upendo wake kwa Kristo na Kanisa.

Mwenyeheri Paulo VI aliandika mwenyewe kwamba, ameitwa na Kristo ili kuliongoza Kanisa si kwa sababu alikuwa na sifa za pekee kabisa, au kuliokoa Kanisa kutoka katika matatizo lililokuwa linakabiliana nayo, bali aweze kuteseka kwa ajili ya Kanisa kwa kutambua kwamba, Yesu mwenyewe ndiye anayeliongoza na kuliokoa.

Hapa unaonekana unyenyekevu wa Mwenyeheri Paulo VI, wakati ambapo ulimwengu ulikuwa unapamba moto na kuongezeka kwa kinzani, akatambua namna ya kuliongoza Kanisa kwa hekima na wakati mwingine katika hali ya upweke; akawa ni nahodha shupavu katika kuliongoza Jahazi la Mtakatifu Petro bila kutindikiwa furaha na imani kwa Yesu Kristo.

Mwenyeheri Paulo VI alifanikiwa kumpatia Mungu yale yaliyokuwa ya Mungu, kwa kujisadaka maisha yake yote kwa ajili ya mambo matakatifu na changamoto zilizokuwa zinaendelea kujitokeza katika nyakati dhdi ya utume wa Kristo. Aliendelea kulipenda na kuliongoza Kanisa ili kweli liweze kuwa Mama mpendelevu na mgawaji wa wokovu kwa watu wote.







All the contents on this site are copyrighted ©.