2014-10-20 08:00:08

Mwenyeheri Papa Paulo VI


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha kanisa la Nyumbani, tumsifu Yesu Kristo. Leo ninakujulisha habari njema ya furaha kubwa sana kwa Kanisa Takatifu ya Mungu na kwa ulimwengu mzima. Jumapili iliyopita tarehe 19.10.2014, Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Papa Paulo VI kuwa mwenye heri. Ni utukufu kwa Mungu na utakatifu wa Kanisa, mama Kanisa anapojipatia mashujaa hawa wa imani kuandikwa katika orodha ya wenye heri. RealAudioMP3 RealAudioMP3

Kwa nafasi hii naomba nikukumbushe kwa kifupi sana mchakato wa kuwatangaza wapendwa wa Mungu kuwa wenye heri na hatimaye watakatifu. Kumtangaza mtu kuwa mtakatifu ni mchakato. Mchakato huu unaongozwa na Imani Takatifu, taratibu-kanuni za jumla na za kipekee. Mama Kanisa anazo taratibu maalumu za kufuata hata mtu aliyeitwa kutoka dunia hii, aweze kutangazwa kuwa Mtakatifu.

Baada ya kufariki mtu, na kisha kuona baadhi ya ishara na miujiza, inayosindikizwa na aina ya maisha ambayo huyo mtu aliishi na aina ya kifo alichokufa, kisha kupita miaka mitano baada ya kufariki, ndipo wahusika huweza kuanza kuomba ruhusa kutoka kiti kitakatifu ya kuanza mchakato wa kumtangaza mtu kuwa ni mtakatifu. Ruhusa hiyo huweza kuombwa na wanandugu au kundi la waamini, au shirika la kitawa kama alikuwa mtawa, au ofisi maalumu ya Kanisa kwa upande wa mababa watakatifu.

Ruhusa hiyo inaombwa kupitia kwa askofu Jimbo, kule alikoishi au kufia mtu huyo. Kiti kitakatifu kikishakutoa ruhusa kwamba mchakato uendelee, basi kwa uruhusisho huo huyo aliyefariki haitwi tena marehemu, bali ni MTUMISHI WA MUNGU.

Baada ya uruhusisho huo, kamati maalumu ya watu wenye imani thabiti na wenye kujua thamani ya ukweli mbele ya Mungu, huanza kukusanya ushahidi juu ya maisha ya Mtumishi wa Mungu. Hapa kuna ushahidi wa maandishi kama aliyaacha, maneno aliyokuwa anatamka (masimulizi kutoka kwa watu), matendo yake ya kiimani kama vile maisha ya sala, sadaka na majitoleo; matendo yake ya upendo kwa jirani.

Hayo yote hukusanywa na kuhakikiwa na ile kamati maalumu ngazi ya jimbo. Nayo huwakilisha uhakiki wao tena kwa Askofu Jimbo. Kwa kuwa Askofu jimbo ndiye mwenye wajibu msingi wa kuwaongoza waamini wake kwa Mungu, yeye ndiye mwenye mamlaka ya kutoa ruhusa ya mchakato kuendelea.

Kisha hakikiwa na Askofu Jimbo, taarifa zote za Mtumishi wa Mungu hupelekwa tena katika Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Nako huko taarifa hizo huhakikiwa kwa Kanuni maalumu zinazoongozwa na Imani kwa Mungu na Kanisa lake katika Kristo Yesu. Taarifa hiyo ikiwa haina mawaa, hupelekwa kwa Baba Mtakatifu, naye kwa uwezo wa kimungu kama Wakili wa Kristo kwa mamlaka ya kimungu aliyo nayo, huhukumu uhalali wa taarifa ya Mtumishi wa Mungu.

Endapo taarifa hiyo itakuwa ni matendo mema ya ushuhuda na ushujaa wa imani, basi Baba Mtakatifu ataidhinisha huyo Mtumishi wa Mungu awe mheshimika. Na hivyo kanisa mahalia huweza kuanza tu kumheshimu.

Huyo Mtumishi wa Mungu, akitenda walao muujiza mmoja, muujiza huo huhakikiwa na kamati ya Imani na wanasayansi, ili kuhukumu kuwa kweli ni muujiza, ni nguvu ya Mungu imetendeka, iwe katika uponyaji au jambo lolote. Muujiza huo hudhihiridha nguvu ya Mungu inayotenda kazi kwa njia ya Mtumishi wa Mungu. Taarifa hiyo ya Muujiza, hupelekwa tena katika kiti kitakatifu. Kiti kitakatifu kikiridhia uhalali wa muujiza au miujiza hiyo, hupeleka taarifa yote kwa Baba Mtakatifu. Na Baba Mtakatifu naye kwa nguvu ya kimungu na uwezo aliopewa, huhukumu na kumtangaza Mtumishi wa Mungu kuwa Mwenyeheri.

Hiyo ndiyo hatua aliyofikia mpendwa na Kiongozi wa Kanisa letu, Wakili wa Kristo na mrithi wa Mtume Petro, PAPA PAULO VI. Kwa ufupi sikia historia yake. Alizaliwa tar 26.09.1897 na kubatizwa kwa jina la Giovanni Battista Montini. Mwaka 1954, alifanywa kuwa Askofu Mkuu wa Milano (Italia). Mwaka 1958, Papa Yohane XXIII alimfanya kuwa Kardinali. Na mwaka 1963, alichaguliwa kuwa Wakili wa Kristo, Mrithi wa Mtume Petro, Kiongozi wa Kanisa Takatifu duniani na Baba Mtakatifu wa wote akichukua jina la Paulo VI, kuashiria dira ya utumishi wake kwa mataifa yote.

Aliliongoza Kanisa Takatifu kama Papa kuanzia tarehe 21 Juni 1963 hadi kifo chake hapo mwaka 1978. Alimrithi Papa Yohane XXIII, aliyeitisha Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Naye akauitisha upya Mtaguso huo, ambao kwa kadiri ya taratibu-kanuni za Kanisa letu, mtaguso ule ulijifunga kufuatia kifo cha Papa Yohane XXIII. Mtaguso huo wa kipekee uliokuwa na lengo na kufungua madirisha na kuleta hewa mpya ndani ya maisha na utume wa Kanisa.

Baada ya vikao vya majadiliano na maamuzi mengi, Mwenyeheri Papa Paulo VI aliufunga Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican mwaka 1965, na yeye ndiye aliyeanza kwa nguvu zote utekelezaji wa mageuzi na maamuzi mbalimbali ya Mtaguso huo muhimu sana.

Kwa kifupi, Papa Paulo VI alikuwa na Ibada timilifu kwa Mama Bikira Maria, upendo wa dhati kwa Kanisa na watu wote. Ndiye aliyemtangaza Mama yetu Bikira Maria kuwa Mama wa Kanisa, wakati wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Alifungua milango ya majadiliano na watu wa dini nyinginezo na wanakaMungu pia. Alijiona kuwa ni mtumishi mnyenyekevu wa wanadamu wateswa.

Kwa dira hiyo, yeye ni Papa wa kwanza kuzungukia nchi za dunia nje ya Italia. Alifanya takribani ziara 16 nje ya Italia, akihubiri amani kwa dunia, haki ya kijamii, njaa duniani, ujinga, udugu wa wanadamu chini ya Mungu na ushirikiano wa kimataifa.

Baada ya kutumikia utume wa mateso kwa muda, tarehe 06.08.1978 katika sikukuu ya kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristu, Baba Mtakatifu Paulo wa VI aliitwa nyumbani kwa Baba wa milele. Kadiri ya matashi yake manyenyekevu sana, alizikwa ardhini katika makaburi ya mapapa yaliyoko chini ya Basilika la Mtume Petro. Ni mazishi yaliyoalika huruma na kugusa mioyo ya wengi sana.

Mchakato wa kumtangaza Papa Paulo VI kuwa ni Mwenyeheri ulianza 11.05.1993. Na tarehe 20.12.2012 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, alithibitisha maisha-shujaa adilifu ya Mtumishi huyo wa Mungu. Muujiza alioutenda mheshimika huyo wa Mungu, ulihakikiwa na Papa Francisko tarehe 09.05.2014. Na Jumapili iliyopita tarehe 19.10.2014 ametangazwa kuwa MWENYEHERI. Taratibu nyingine zitaendelea, kwa msaada na huruma ya Mungu atangazwe kuwa MTAKATIFU. Katika kipindi kijacho, tutakuletea kwa kifupi, makuu aliyoyatenda, mintarafu Mtaguso wa II wa Vaticani. Mwenye heri Papa Paulo VI – Utuombee.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.