Jumuiya ya Kimataifa inashuhudia vitendo vya kigaidi ambavyo havijawahi kutokea hata
kidogo!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 20 Oktoba 2014 ameongoza mkutano wa Makardinali,
ili kutafakari maombi yaliyowasilishwa kwake na Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini
kuwa wenyeheri na watakatifu, ili Mwenyeheri Giseppe Vaz na Maria Christina wa Bikira
Maria Mkingiwa dhambi ya asili waweze kutangazwa na Mama Kanisa kuwa ni watakatifu.
Papa Francisko ametumia fursa hii pia kuzungumzia kuhusu hali Mashariki ya Kati, lakini
zaidi kuhusu dhuluma na nyanyaso wanazokabiliana nazo Wakristo huko Mashariki ya Kati.
Baba Mtakatifu anasema, watu wengi wana kiu ya kutaka kuona amani inatawala
tena huko Mashariki ya Kati pamoja na utashi wa kutaka suluhu ya kudumu iweze kupatikana
ili kumaliza mapambano ya vita kwa kujikita katika majadiliano, upatanisho na utekelezaji
wa mikakati ya kisiasa inayoamriwa. Kanisa linapenda kutoa msaada wake kwa Jumuiya
za Kikristo huko Mashariki ya Kati, ili kusaidia mchakato wa kuendelea kubaki katika
maeneo yao ya asili.
Baba Mtakatifu anasema, haiwezekani kufikiri Mashariki
ya Kati bila ya uwepo wa Wakristo, ambao kwa takaribani miaka elfu mbili wameendelea
kuungama imani juu ya Yesu Kristo. Matukio ya hivi karibuni huko Iraq na Syria yanasikitisha
sana, kwani Jumuiya ya Kimataifa inashuhudia kwa macho makavu vitendo vya kigaidi
ambavyo havijawahi kutokea.
Kuna maelfu ya watu wanaodhulumiwa, kiasi kwamba,
wanalazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Hapa inaonekana
kana kwamba, utu na heshima ya binadamu havina thamani tena, kiasi hata cha kuwatoa
watu wengine sadaka kwa ajili ya mafao binafsi na jambo la kushangaza ni kuona kwamba,
watu wengi hawaguswi na mahangaiko ya watu hao.
Baba Mtakatifu anasema hali
hii inahitaji waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kujikita katika sala
na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutoa majibu muafaka. Ni matumaini ya Baba
Mtakatifu Francisko kwamba, mkutano wa Makardinali utasaidia kupata mawazo na majibu
yatakayoliwezesha Kanisa kutoa msaada unaohitajika kwa ajili ya Jumuiya za Kikristo
huko Mashariki ya Kati, chimbuko la Ukristo!