Serikali ya Vietnam inalipongeza Kanisa kwa kushiriki katika ustawi na maendeleo ya
wananchi wa Vietnam
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi mchana alikutana na kuzungumza na Bwana Nguyen
Tan Dung, Waziri mkuu wa Vietnam ambaye baadaye pia alikutana na Kardinali Pietro
Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Dominique Mamberti,
Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Baba
Mtakatifu na mgeni wake wamepongeza hatua ambayo imefikiwa kati ya nchi hizi mbili
katika mchakato wa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili tangu Waziri mkuu wa
Vietnam alipotembelea kwa mara ya kwanza Vatican kunako mwaka 2007. Vietnam inalishukuru
Kanisa kwa mchango wake katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Vietnam katika ujumla
wao. Kanisa linaishukuru Serikali kwa ushirikiano uliopo mintarafu Katiba ya nchi
ya Mwaka 2013 katika masuala ya kidini.
Mwakilishi wa Vatican nchini Vietnam
asiye mkazi ameendelea kuchangia kwa karibu zaidi katika kukuza mahusiano mema kati
ya Serikali na Kanisa, wakilenga zaidi katika kuimaarisha ushirikiano wa kidiplomasia.
Viongozi hawa wawili kwa pamoja wamejadili masuala msingi yatakayofanyiwa kazi na
pande hizi mbili katika siku za usoni kwa kuendelea kutumia njia za mawasiliano zilizopo
hadi wakati huu.
Baba Mtakatifu na mgeni wake, wamebadilishana mawazo kuhusiana
na masuala mbali mbali yanayoendelea kutikisa Kikanda na Kimataifa, lakini kwa namna
ya pekee wameangalia sera na mikakati inayochukuliwa na Jumuiya ya Kimataifa katika
kujenga na kudumisha misingi ya amani na utulivu Barani Asia.