2014-10-19 14:50:34

Mwenyeheri Paulo VI alikuwa mhimili mkuu katika mchakato wa Uinjilishaji


Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko alitumia fursa hii kuwasalimia waamini na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliofika mjini Vatican kushuhudia Mababa wa Sinodi wakifunga maadhimisho haya, Papa Paulo VI akitangazwa kuwa Mwenyeheri na kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya themanini na nane ya Kimissionari Duniani.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa umati mkubwa wa waamini kutoka Brescia, Milano na Roma; watu ambao wana mahusiano maalum sana katika maisha na utume wa Mwenyeheri Paulo VI. Baba Mtakatifu anawapongneza kwa uwepo wao na anawahimiza kufuata kwa uaminifu mafundisho na mfano wa maisha ya Mwenyeheri Paulo VI.

Papa Paulo VI alikuwa ni mhimili mkubwa katika kusimamia mchakato wa Uinjilishaji wa watu; ushuhuda unaojionesha kwa namna ya pekee katika Waraka wake wa "Evangelii nuntiandi" unaoamsha mikakati ya na utume wa Kanisa katika kutangaza Injili hadi miisho ya dunia. Hili ni tukio muhimu sana kwa Mama Kanisa hasa wakati huu anapoadhimisha Siku ya themanini na nane ya Kimissionari Duniani.

Baba Mtakatifu Francisko amekiri kwamba, Mwenyeheri Paulo VI alikuwa na Ibada maalum kwa Bikira Maria na kwamba, ataendelea kukumbukwa na Watu wa Mungu kwa mafundisho yake ya kina kuhusu Bikira Maria katika Waraka wake "Marialis cultus", yaani Ibada kwa Bikira, kwa kutangaza kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa, wakati alipokuwa anafunga awamu ya tatu ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu anawaombea waamini wote ili Bikira Maria aweze kuwasaidia kuwa kweli ni waaminifu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao kama alivyofanya Mwenyeheri Paulo VI.







All the contents on this site are copyrighted ©.