2014-10-19 10:36:40

Mshikamano wa kimataifa unahitajika kupambana na ugonjwa wa Ebola


Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola bado yanaendelea Barani Afrika, lakini yanahitaji ushiriki wa Jumuiya ya Kimataifa, ili kuchangia rasilimali fedha na vifaa tiba vinavyohitajika kwa wakati huu. Wasi wasi wa kuenea kwa ugonjwa wa Ebola sehemu mbali mbali za dunia unazidi kuongezeka kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa ukamilifu zaidi, ili ugonjwa huu uweze kutokomezwa.

Ni maoni ya Bwana Jim Yong Kim, Rais wa Benki ya Dunia, anayekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha mshikamano katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola, kwani ni ugonjwa ambao una madhara makubwa kwa uchumi, ustawi na maendeleo ya watu wengi duniani. Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya pamoja na taasisi za kimataifa zimeamua kushikamana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola, kwa kuwa na mawazo na mwono mpana zaidi unaovuka mipaka ya watu katika maeneo husika.

Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuchagia rasilimali watu, vifaa na fedha katika mapambano dhidi ya virusi vya Ebola vinavyoendelea kuwa ni tishio kwa maisha na usalama wa watu wengi duniani. Taarifa zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna wagonjwa 4, 555 waliofariki dunia na kuna watu 9, 216 katika nchi saba wamekwisha ambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ebola. Nchi ambayo hadi sasa imeathirika kwa kiasi kikubwa ni Liberia, Guinea, Siera Leone na Nigeria. Kuna watu wameonesha dalili za kuwa na virusi vya Ebola nchini Senegal, Marekani na Hispania.







All the contents on this site are copyrighted ©.