2014-10-17 07:52:49

Kanisa linapenda kuwatangazia watu ukweli kuhusu utakatifu wa maisha ya ndoa na familia!


Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha umuhimu wa Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia iliyoanza kuadhimishwa hapo tarehe 5 Oktoba na inafungwa rasmi Jumapili tarehe 19 Oktoba 2014 kwa Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko sanjari na kumtangaza Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI kuwa Mwenyeheri. Hii ni Siku ya 88 ya Kimissionari Duniani. RealAudioMP3

Umuhimu wa maisha na utume wa Familia anasema Askofu mkuu Lebulu unajikita katika maisha halisi ya wanandoa na familia na wala si katika nadharia na hali ya kufikirika, changamoto kubwa ni kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa wanandoa ili waweze kushiriki kikamilifu katika utume na maisha ya Kanisa sanjari na kujipatia neema kwa kushiriki Sakramenti za Kanisa. Kuna baadhi ya wanandoa wanakabiliwa na changamoto ya kuishi kikamilifu Sheria,Kanuni na Mapokeo ya Kanisa.

Mama Kanisa, Mama na Mwalimu anapaswa kuwasaidia wanandoa hawa kuishi kikamilifu Ukristo wao, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Sheria, Kanuni na Mapokeo ya Kanisa yaangaliwe kwa umakini mkubwa mintarafu hali halisi ya wanandoa na familia, kwani Kanisa linapaswa kuwasaidia kweli wanandoa kuishi Ukristo wao licha ya mapungufu yao ya kibinadamu.

Sheria na Kanuni za Kanisa ziwasaidie kuwatetea wanyonge na kuwasaidia kupata maisha ya uzima wa milele. Waamini wote wawe ni wadau katika azma ya Uinjilishaji kwa kutambua kwamba, Familia kweli ni kitovu cha Uinjilishaji.

Kwa upande wake Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anayeshiriki katika maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia anawaalika waamini wote kuendelea kusali kwa ajili ya kuwaombea Mababa wa Sinodi wanatekeleza wajibu na dhamana hii nyeti.

Ni matumaini ya Mababa wa Sinodi kwamba, wataipatia Familia ya Mungu ujumbe wa imani, matumaini na mapendo unaojikita katika ukweli na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia. Lengo ni kuliimarisha: Familia, Kanisa na Jamii ya binadamu, ili iweze kupata neema na baraka tele kutoka kwa Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.