2014-10-16 09:03:42

"Wanatikisa kibiriti, Yesu anawatolea uvivu"!


Wakati wa Yesu kulikuwa na makundi ya watu yenye itikadi za kidini na kisiasa zinazopingana. Kati ya makundi hayo kulikuwa Wafarisayo na Maherodi. Makundi haya mawili tungeweza kuyalinganisha na vyama vya upinzani vyenye itikadi na sera tofauti za kisiasa katika nchi.

Leo tutawaona viongozi wa vyama hivyo wakiungana pamoja ili kuihujumu serikali. Watu wa vikundi hivyo vya Wafaisayo na Maherodi pamoja na mashabiki wao wakamwendea Yesu mtu wa kweli na haki kama wanavyoanza kumrubuni kwa lugha nzuri wanamwambia: “Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu.” Baada ya kumwagia sifa hizo ili ashabikie ufisadi wao wakamwuliza swali la kifisadi: “Basi utuambie, waonaje ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?”

Katika Injili ya Luka suala la kodi na ushuru lilikuwa nyeti sana, na ndilo walilomshtakia Yesu kwa Pilato kusudi auawe: “Wakaanza kumshitaki, wakisema, ‘Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo Mfalme.’” (Lk.23:2) Swali hili lilikuwa na mtego ulio mgumu sana kuuepa, kwani lilimbana Yesu katika masuala mawili mazito na nyeti yanayoikabili kila nchi yaani katika uwanja wa kiuchumi na wa kisiasa.

Ingawaje ulipaji kodi au ushuru ni suala la toka zamani za mababu zetu lakini zoezi hili limebaki kuwa nyeti na linalokera sana wananchi popote ulimwengu, hasa kutokana na jinsi linavyogusa uchumi binafsi. Kwa hiyo kutokana na unyeti wake, suala hili linasababisha kuwa na migomo na maandamano ya mara kwa mara katika nchi. Kuhusu kero hiyo ya ulipaji wa kodi tunaweza kuiona kidogo tukifuatilia makala ya mwanahistoria myahudi Yosefu Flavio, aliyeishi kipindi walichokuwa wanaishi mitume.

Mwanahistoria huyu anasimulia vituko mbalimbali ambavyo viliwahi kutokea huko Palestina wakati wake, vituko vilivyoibua migomo na maandamano kadhaa kule Palestina dhidi ya ulipaji kodi kwa serikali ya kikoloni. Ananukuu kituko kile cha Yuda wa Galla kinachosimuliwa pia katika kitabu cha Matendo ya Mitume, kulipokuwa na sensa ya Kwirinus, kwa ajili ya kujua idadi ya watu wa kulipa kodi.

Suala lenyewe la kuhesabu watu halikukubalika kwa Wayahudi, hata Daudi anaomba radhi kwa kosa hilo, kwani ni Mungu peke yake anayo mamlaka juu ya mtu kwa sababu hakuna mtu yeyote duniani mwenye mamlaka juu ya mwingine. Ulipaji kodi uyahudini ulileta maudhi zaidi kwa vile uligusa itikadi ya dini yao, kwani katika sarafu ya fedha kuliandikwa maneno yaliyo kinyume na imani kwa Mungu mmoja. “….” Upande wa pili “Sommo Pontefice” na picha ya mwanamke aliyekaa, alama ya amani, yawezekana mwanamke huyo alikuwa ni mama wa mwenyewe Tiberius. Kwa wayahudi kuitumia sarafu hiyo ilikuwa kama kuabudu miungu ya uongo.

Katika mazingira kama hayo, ndiyo linaingia swali la mafisadi hao ili wamwingize Yesu mkenge, yaani wamgonganishe na utawala (kwa kutolipa kodi), na aingilie kuchafua utaratibu wa uchumi. Huo ni ufisadi kwani unataka kumpa mtu mwanya wa kuepa wajibu wake wa kulipa kodi kwa serikali. Aidha ni swali la kisiasa kwa vile linataka kumgombanisha Yesu na Kaisari pamoja na taifa lake la wayahudi.

Kwa vyovyote Mafisadi hawa walijua wazi kwamba wanawajibika kulipa kodi kwa serikali yao, lakini kwa bahati mbaya serikali yao ilikuwa ya wakoloni wa kirumi. Walilazimika kulipa kodi chini ya utawala wa warumi tena kwa kutumia pesa ya nuksi kwani ilikuwa na sura ya mfalme Tiberius aliyejidai kuwa mungu.

Kwa vile ni swali la kihuni, Yesu naye anacheza na uhuni wao bila wao kujitambua. Anaomba kuoneshwa sarafu ya pesa. Kwa kufanya hivyo yaonesha kwamba yeye mwenyewe alikuwa fukara, hakuwa na pesa mfukoni. Lakini wao walikuwa nayo na walikuwa wanaitumia ndiyo maana wanachomoa mifukoni mwao na kumpa. Mbaya zaidi walikuwa katika mazingira ya hekaluni (kanisani) sehemu takatifu (Mt. 21:23).

Hawaogopi kutia nuksi Kanisani kwa kuonesha pesa yenye picha ya mfalme Kaisari. Hapo wanaonesha jinsi walivyo wanafiki kwa sababu wanakuwa na uangalifu tu wanapotakiwa kulipa kodi na ushuru. Yesu baada ya kuichunguza pesa ile, anawauliza: “Ni ya nani sanamu hii?” Wanapomjibu kuwa ni ya Kaisari, anawaambia: “Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu.” Jibu hili la Yesu linajulikana na watu wote hata wasio wakristu, hasahasa wana siasa na watu wa serikali, na wanafasiri kadiri inavyowapendeza wao.

Hao wanasema kuwa Yesu alimaanisha kuwa “dini isiingilie mambo ya serikali na siasa” na watu wa dini wanasema kwamba Yesu alimaanisha kwamba dini inamwakilisha Mungu na hivi inayo mamlaka hata upande wa siasa na dini.” Hebu tuone Yesu mwenyewe alimaanisha nini.

Kuna ujumbe au mafundisho mawili yayopatikana katika jibu hili: Mosi, ni dhahiri kabisa kwamba, kulipa kodi ni wajibu wa kimaadili licha ya wajibu wa kiraia kuchangia kutokana na tunachotendewa na jamii hiyo. Hakuna hoja yoyote ya haki au utetezi wowote ule wa kutolipa kodi au ushuru. Hata kama uongozi wa serikali ungekuwa ovyo na wa kidhuluma.

Kumbe, kiuchumi na kisiasa, wanafunzi wa Kristo wameitwa kuwa raia waaminifu na wenye kutoa mfano wa kuwajibika katika kujenga jamii yenye haki na upendo. Mkristo daima achague siasa inayowapendelea zaidi wanyonge, siyo ile inayohifadhi maslahi yake tu.

Ndiyo maana Paulo anawaandikia warumi- katika kipindi ambacho Roma ilikuwa imeanza kutawaliwa na mfalme Nero – akiwa bado kijana tu wa miaka 20 tu na kwa muda kidogo wa miaka mitatu ya utawala wake, anawahimiza wakristu wa Roma akisema: “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo imeamriwa na Mungu.

Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu…Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri. Kwa sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi hiyo hiyo. Wapeni waote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima;” (War. 13:1-7).

Kwa jibu hilo Yesu anataka kutuasa juu ya kuwajibika, yaani, kama umepewa huna budi kurudisha. Kama umepokea, yabidi kurudisha. Ninyi mnatumia hela iliyo mali ya serikali ya kirumi. Serikali hiyo inawatengenezea barabara, inawahakikishia usalama wa raia, yaani ina askari wanaowalinda, inawaendeshea biashara, na mambo yanaenda sawa. Mmepokea haya yote sasa rudisheni, maana yake lipeni kodi zote kutokana na huduma mnayopata hakuna hoja ya kuepa kulipa kodi au ya kutokutoa ushuru.

Kwa hiyo siyo hakikuepa kutoa ushuru ba kulipa kodi. Tunaweza pia kuwaasa mafarisayo wa leo wanaoepa kulipa kodi na kutoa ushuru. Kumbe unawajibika “kurudisha” yaani kulipa kodi kwa sababu unalo deni kwa serikali inayokuhudumia. Nikifikiria kile ambacho nimepokea, katika uwanja wa elimu, wa afya, na mambo gani nimewahi kupata bure, kadhalika nimepata zaidi ya kile ninachoweza kutoa.

Kadhalika ninalo deni kubwa kwa wazazi, kwa marafiki, kwa walimu, kwa yule aliyenifundisha imani, kwa aliyenipa upendo, kwa wale wanaoleta maendeleo, ama kweli mimi nimebaki kuwa kama kipande tu cha madeni. Haitoshi tu kuuliza: eti wewe unafikiri nini juu ya nchi yetu? Bali yatakiwa kuuliza: wewe utairudishia kitu gani jamii yetu?

Unafanya nini ili kuninusuru nchi yetu na ubadhilifu na rushwa, na uonezi na magomvi. Ushirikiano wa kwanza ni ule wa kulipa kodi. Kwa kufanya hivyo, utawafundisha hata wale wajeuri wengine wanaodanganya jamii na kunyonya taifa na kuwanyonya wanyonge.

Swali zito kwa mkristu lingekuwa ni namna gani mmoja anaweza kumrudishia au kumpa kodi Kaisari mkoloni (mbaya) au Kiongozi fisadi (yaani viongozi wevi na wachakachuaji) ambao sina imani nao kabisa. Yaani kulipa kodi kwa serikali badhilifu. Katika hali kama hiyo ndipo inapoingia sifa ya Yesu, ya kutokutazama uso wa yeyote, kama walivyosema wapinzani wake: “twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na hutazami sura za watu.”

Kwa hiyo, kuwajibika kwa Kaisari au viongozi fisadi wanaoiba maana yake ni kumpa kodi au ushuru wake, yaani kumpa ukweli anaostahili, kumpa ile sauti ya ukweli na uwazi itakayomkereketa dhamiri na kumwajibisha ili awe mtu wa kutenda haki. Kama jinsi vyombo vya habari, au vyama mbalimbali vya kisiasa na dini vinavyoikosoa serikali ili ovyo.

Huo ndiyo ushuru na kodi ninayowajibika kumlipa Kaisari au kiongozi mbadhilifu. Kwa hiyo dini haiingilii mambo ya serikali na siasa bali sehemu ya wajibu wake kwa Kaisari.

Baada ya kuwajibika hivyo kwa Kaisari, kwa serikali na kwa viongozi, kunafuata kuwajibika kwa Mungu. Mpe Mungu yaliyo ya Mungu. Mosi, sisi binadamu tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Sisi ni tuko kama sanamu, picha, sura ya Mungu. Kumrudishia Mungu yaliyo yake, maana yake tuoneshe kama kweli kuwa tu hiyo picha ya Mungu wa amani, wa haki na upendo kwa wote. Kama vile tunavyosafisha picha zetu zinapokuwa na vumbi, ndivyo nasi tujikosoe na kujisafisha tuwe safi dhidi ya uovu ili daima tuakisi uzuri wa Mungu ulio ndani yetu.

Pili, Wafarisayo walikuwa wanatunza mifukoni mwao pesa ya Kaisari, na wanaambiwa wamrudishie pesa yake. Kadhalika yaonekana wameshikilia pia kwa namna isiyo sawa mali, mamlaka, na haki za Mungu, basi wanaambiwa mamlaka, na mali zote ni haki ya Mungu, basi wamrudishie. Wamwachie Mungu kupata heshima yake Mungu wasimpore heshima yake.

Kwa lugha hiyo, Yesu alitaka kumpokonya au kumvua Kaisari cheo cha kimungu, na kutenganisha kabisa vyeo hivi, na “kumwacha Kaisari aitwe biandamu na Mungu aitwe Mungu” Kwa hiyo, “Kumpa Mungu yaliyo ya Mungu” maana yake Kaisari apewe vitu, lakini Mungu apate watu, nafsi na heshima yake yote, na ukuu wake wote, dhamiri yake, moyo wake.

Kwangu Yesu anasema: usiandike kitu kingine moyoni mwako zaidi ya Mungu. Uwe huru na aina yoyote ile ya mawazo, makusudio, usitawaliwe na chochote; uyakatalie mamlaka hayo hayakuhusu. Kwa kila mamlaka ya kibinadamu Yesu anasema: Usimtawale binadamu, usitawale dhamiri ya binadamu. Binadamu anamhusu Mungu, ni kitu au nafsi ya Mungu. Mtu anaye Mungu katika damu. “Mwache Kaisari awe Kaisari na Mungu aitwe Mungu.”

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.