2014-10-16 10:14:29

Siku ya chakula duniani kwa mwaka 2014


Familia za wakulima zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuulisha ulimwengu ni kundi linalopaswa kulinda na kutunza mazingira, kwani hili ni kundi muhimu sana katika mchakato wa mikakati endelevu ya kuwa na usalama wa chakula.

Jumuiya ya kimataifa inaadhimisha Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2014, huku kukiwa na dalili za kupungua kidogo kwa watu wanaokabiliwa na baa la njaa dunia na kwamba, kuna nchi sitini na tatu ambazo tayari zimeonesha mafanikio katika kupunguza idadi ya watu wanaoteseka kwa lishe duni, lengo ni kung'oa kabisa baa la njaa duniani.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Bwana Ban Ki-moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, inayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe 16 Oktoba. Bado Jumuiya ya Kimataifa haina budi kulivalia njuga baa la njaa, kwani hadi sasa bado kuna watu millioni mia nane wanaokabiliwa na upungufu wa chakula na lishe duni na kwamba, kuna watoto wanaokumbwa na utapiamlo; mambo yanayochangia kudumaa kwa shughuli nyingi.

Familia za wakulima ni chachu ya maendeleo ya kimataifa, lakini kwa bahati mbaya wanakabiliwa na ukosefu wa teknolojia, huduma na masoko ya uhakika. Ni kundi ambalo linaathirika kutokana na hali ya hewa, mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira. Wakulima wadogo wadogo zaidi ya millioni mia tano, ikiwa kama watawezeshwa kikamilifu wanaweza kuchangia katika mchakato wa kuung'oa umaskini sanjari na kutunza mazingira.

Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kupembua kwa kina na mapana anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kuwekeza katika sekta ya kilimo na uvuvi pamoja na kudhibiti mabadiliko ya tabia nchi. Changamoto ya kupambana na baa la njaa pamoja na kupata lishe bora, ni mambo makuu mawili yanayozihamasisha Serikali, vyama vya kiraia na sekta binafsi kushirikiana kwa ukaribu zaidi. Kuna mafanikio makubwa katika uhakika wa usalama wa chakula duniani kwa kujitahidi kuokoa chakula kinachotupwa kila mwaka sanjari na kuendeleza mfumo wa kilimo cha umwagiliaji maji na uvuvi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anabainisha kwamba, Mwaka 2015, Jumuiya ya Kimataifa inapania kufanya mageuzi makubwa kwa kuangalia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia pamoja na udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabia nchi. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuona ulimwengu pasi na baa la njaa, kwa kushiriki haki ya kupata lishe bora, ili kujenga ulimwengu bora zaidi. Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, iwe ni fursa ya kujikita katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.