2014-10-13 14:07:31

Jifungeni kibwebwe kupambana na baa la njaa na utapiamlo!


Bwana Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO anasema, Jumuiya ya Kimataifa imepiga hatua kubwa katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanakuwa na uhakika wa chakula bora. Hii inatokana na mazungumzo ya kina yaliyofanyika kati ya Shirika la Afya Duniani, WHO na FAO, hata kufikia mapendekezo 50 ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa ili kuweza kufikia lengo hili.

Mapendekezo yaliyotolewa yatafanyiwa kazi katika mkutano mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu lishe, unaotarajiwa kufanyika mjini Roma kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 21 Novemba 2014. Ni mkutano utakaowashirikisha viongozi wakuu kutoka FAO na Shirika la Afya Duniani, lengo ni kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na lishe bora duniani.

FAO inakadiria kwamba, kuna jumla ya watu millioni 805 wanaokabiliwa na baa la njaa duniani na kwamba, nusu ya idadi ya watu duniani wanasumbuliwa na tatizo la utapiamlo, mambo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kudhorotesha afya ya watu wengi duniani. Baa la njaa na utapiamlo unasababisha madhara makubwa katika maendeleo ya jamii na athari katika ukuaji wa uchumi katika nyanja mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza zaidi katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo duniani ili kudhibiti pia umaskini wa hali na kipato, tayari kuwajengea watu uwezo wa kuboresha maisha yao. Hii ni dhamana inayopaswa kufanyiwa kazi kwanza kabisa na Serikali husika kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, ili kufikia malengo yanayokusudiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Ni changamoto ya kuendelea kuboresha uzalishaji katika sekta ya kilimo, ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani. Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kupunguza vifo vya watoto wadogo kwa kiasi kikubwa.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna jumla ya watoto zaidi ya millioni 160 wenye umri chini ya miaka mitano wanaokabiliwa na utapiamlo wa kutisha, hali inayodumaza makuzi na maendeleo ya watoto hawa. Wakati huo huo, kuna watoto nusu billioni wanaokabiliwa na uzito wa kutisha. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wakuu wa mashirika ya kimataifa na wakuu wa nchi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huu maalum kama sehemu ya mchakato wa kupambana na baa la njaa na utapiamlo duniani.







All the contents on this site are copyrighted ©.