2014-09-19 15:39:45

Tafakari ya Neno la Mungu Domonika ya 25 ya Mwaka A,



Mpendwa, tunatafakari masomo ya Jumapili ya 25 ya mwaka wa A wa Kanisa, tukialikwa kuwa na matumaini daima katika kumtafuta Bwana na kutambua kuwa wema wa Mungu ni wa milele kwa watu wote na fikra zake ni tofauti na fikra za kibinadamu. Katika somo la kwanza Waisraeli wako utumwani Babeli kwa sababu hawakutii mausia ya Bwana na zaidi wanaona hawawezi kusamehewa dhambi zao, wamepoteza tumaini na wanaona kana kwamba Mungu amewatupa na kuwaacha kabisa. Zaidi ya hilo wanaongeza kosa jingine tena la kumwona Mungu anayefikiri kama wao, wanafikiri hawezi kuwasamehe tena.


Mpendwa, katika shida yao hiyo Mungu anamtuma Nabii Isaya awaambie kuwa fikra na njia za Mungu ni za juu mno ni tofauti na fikira za kibinadamu kiasi kwamba si rahisi kuzielewa. Zaidi ya hilo Isaya anawakumbusha kuacha njia zao mbaya na kumrudia Bwana. Kumrudia Bwana si tu kuacha dhambi, bali pia kubadili namna ya kumtazama Mungu, Mungu aliye haki na mkamilifu. Mawazo haya yatajitokeza waziwazi katika Injili ambapo tunaona Mungu anayewapenda wote wadhambi kwa wema.


Mtume Paulo akikoleza ujumbe wa nabii Isaya anawaambia Wafilipi, hata kama kuna shida katika maisha yao watambue kuwa kuishi kwao ni Kristu, ndiyo kusema la maana katika maisha yao ni Kristu mfufuka. Mara kadhaa watu wapatapo shida huanza manunguniko dhidi ya Mungu na kusahau kwamba yote waliyonayo yametoka kwake. Wanasahau kuwa, kwa njia ya msalaba yaani njia ya mateso, Kristu ametustahilisha kwenda mbinguni. Ndiyo kusema, hata sisi tuliodhaifu tunapaswa kupitia njia ya mateso ili kuweza kufika Mbinguni. Kwa hakika mtume Paulo anapoandika barua hii kwa Wafilipi yuko katika wakati mgumu yaani kuchagua kufa ili akae na Kristu au kuendelea kuhubiri Injili kwa mataifa, na mwisho anaona ahitimishe fikra zake akisema kuishi kwangu ni Kristu na kufa ni faida. Hapa tunaonja imani ya Paulo ilivyozama katika Mwana wa Mungu.

Tujiulize je kwetu sisi kuishi na kufa, twaweza kuvipokea kama alama ya ushindi katika imani kama Mtume Paulo? Mpendwa msikilizaji jitafiti na hivi unapokuwa umechoka, unapokuwa umefikia mwisho wa maisha yako uweze kusema nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza na imani nimeilinda sasa kufa kwangu ni faida na kuishi kwangu ni Kristu!


Mpendwa mwana wa Mungu tukiongozwa na mwinjili Mathayo, tunapata kuonja kuwa mawazo ya Mungu ni ya juu sana kuliko yetu. Jambo hili linajionesha wazi katika Injili ya leo pale ambapo Bwana wa shamba anawaajiri watu mbalimbali katika masaa tofauti na mwishoni anawalipa ujira sawa. Mpendwa katika hali ya kawaida, Bwana huyu angepaswa kuwalipa tofauti kwa maana muda wa kazi ulikuwa tofauti. Kuwalipa ujira sawa pia ni namna ya kusema kuwa uvivu uendelee katika ulimwengu, tuseme hakuna ile haki ya kawaida yaani common justice! Hii ni namna yetu ya kufikiri na hata namna ya watu wa wakati huo, lakini je Mwinjili anataka kutuambia nini? Je Bwana afikiri kama sisi?


Kwa hakika kuwalipa ujira sawa maana yake, wema wa Mungu ni kwa ajili ya wema na wabaya. Wale walioajiriwa kwanza ndio walisadikiwa kuwa wema na wale wa baadaye ndio kundi wakilishi la walio wabaya. Pamoja na hilo kuna jambo jingine jema, kwamba mwenye shamba anapenda kila mmoja afanye kazi, asiishi bila wajibu, ajisikie katikati ya jumuiya ya watu kwa maana kazi huleta heshima. Kwa jinsi hiyo kazi ya wokovu inaendelea na inawaletea heshima watu wote.
Mfano huu wa mwenye shamba unatufundisha kuwa Mungu si mhasibu wala meneja anayewalipa watu kulingana na jasho lao tu, bali kulingana na upendo wake aliokusudia tangu alipoumba ulimwengu. Hatuna uwezo wa kupata stahili yoyote toka kwa Mungu kwa nguvu zetu bali kwa uweza wake, huruma yake na mapendo yake ya milele. Kwa wazo hili tunarudi kwa nabii Isaya anayetuambia kuwa njia zake ni za juu mno na mawazo yake hatuwezi kuyafikia. Tunaalikwa kutambua kuwa wokovu si kwa maveterani peke yao bali hata vijana wanaokuja saa kumi na moja jioni! Hakutakuwa na upendeleo wowote katika wokovu cha msingi ni kumtafuta Bwana madamu anapatikana. Tumsifu Yesu Kristu.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps








All the contents on this site are copyrighted ©.